1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upigaji kura umeanza Venezuela

Sekione Kitojo
30 Julai 2017

Rais Nicolas Maduro  wa Venezuela alipiga kura leo Jumapili kuzindua rasmi kura yenye utata nchini humo kulichagua bunge litakalokuwa na nguvu na kuahidi kwamba litaondoa mzozo wa nchi hiyo kwa kuandika katiba mpya.

https://p.dw.com/p/2hOMH
Venezuela Wahlen - Präsident Nicolas Maduro
Rais Nicolas Maduro akipiga kura mjini CaracasPicha: Reuters

Kura  hiyo imekuwa  ikipingwa  sana  katika  miezi  kadhaa  ya maandamano  mitaani  na  kukosolewa  kimataifa.

Upinzani  nchini  Venezuela  unasema  ni juhudi  za Maduro ambaye anakumbwa  na  matatizo kung'ang'ania  madarakani kwa  kuzunguka nyuma  ya  bunge  ambalo  linadhibitiwa  na  upinzani.

Venezuela Wahlen - Präsident Nicolas Maduro
Rais Nicolas Maduro akionesha kura yakePicha: Reuters

Televisheni  ya  taifa  imemuonesha  maduro  akipiga  kura  katika eneo  la  magharibi  mjini  Caracas  kwa  ajili ya  bunge  la  wananchi litakalokuwa  na  wajumbe 545  ambalo  litakuwa  na  mamlaka  ya kulivunja  bunge  linalodhibitiwa  na  wapinzani na kubadilisha  sheria wakati  likifanya  mageuzi  ya  katiba  ya  nchi  hiyo.

"Mimi ndie mpigaji  kura  wa kwanza  nchini. Namuomba  Mungu kwa baraka  zake ili  watu  waweze  kutimiza kwa  uhuru mchakato wa haki  zao  za  kidemokrasia  na  kuweza  kupiga  kura," rais amesema . Aliongozana  na  mkewe, Cilia Flores , ambaye  ni mgombea  ambaye  atakuwamo  katika  bunge  hilo  jipya.

Venezuela Wahlen
Umati wa watu ukisubiri kupiga kura Julai 30,2017Picha: Reuters/U. Marcelino

Idadi  ya  watu  waliojitokeza  itakuwa  muhimu  katika  uchaguzi huo. Upande wa  upinzani  umetoa  wito  wa  kususia  kura  hiyo, ukisema  kura  hiyo  ni  juhudi  za  kumuelekeza  Maduro  katika "udikteta" kwa  kuungwa  mkono  na  jeshi.

Uchunguzi wa maoni ya wapiga kura

Uchunguzi uliofanywa na  kampuni inayochunguza  maoni  ya  wapiga kura  ya Datanalisis unaonesha  kwamba  zaidi  ya  asilimia 70 ya watu  wa  Venezuela wanapinga  wazo  la  bunge  hilo  jipya -- na asilimia  80 wanakataa  uongozi  wa  Maduro.

Miezi  minne  ya  maandamno  ya  mitaani  dhidi  ya  Maduro yamesababisha  zaidi  ya  watu 100 kuuwawa, na  kuweka  wazi mgawanyiko  mkubwa  wa  kisiasa   katika  taifa  hilo  lenye  utajiri mkubwa  wa  mafuta ambalo  hivi  sasa  limetumbukia  katika  hali mbaya  ya  kiuchumi.

Venezuela Wahlen
Wananchi wakisubiri kupiga kura mjini CaracasPicha: Reuters/U. Marcelino

Maandamano zaidi yameitishwa  leo  Jumapili  kwa  ajili  ya  kupinga kura  hiyo, licha  ya  marufuku iliyotolewa  na  Maduro  na  kuamuru kitisho  cha  kuwaweka jela  waandamanaji  kwa  kipindi  hadi  miaka 10.

Lakini  hofu  ya  kuongezeka  kwa  ghasia  imesambaa  katika  eneo hilo, na  hata  kupindukia.

Marekani , Umoja  wa  Ulaya  na  mataifa  makubwa  ya  Amerika kusini , ikiwa  ni  pamoja  na  Argentina, Brazil , Colombia  na  Mexico zimejitokeza  kupinga  kura  hiyo, yakisema  itaharibu demokrasia nchini  Venezuela.

Massenproteste gegen Maduro vor Wahl in Venezuela
Waandamanaji wakipambana na polisi mjini Caracas wakipinga kura hiyoPicha: Picture-Alliance/AP Photo/A. Cubillos

Mashirika  kadhaa  ya  ndege  ya  kimataifa , ikiwa ni  pamoja  na shirika  la  ndege  la  Ufaransa, Delta, Avianca na Iberia yamesitisha  safari  zake  kwenda  nchini  humo kutokana  na  hofu ya  usalama.

Familia  za  wanadiplomasia  wa  Marekani   zimeamuriwa  kuondoka kufuatia  vikwazo  vilivyowekwa  na  Marekani  dhidi  ya  maafisa  13 wa  sasa  na  wazamani  wa  Venezuela.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Isacc Gamba