1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Somalia watangaza kutomtambua rais

John Juma
8 Februari 2021

Viongozi wa upinzani nchini Somalia wametangaza kuwa hawamtambui tena Rais Mohamed Abdullahi Mohamed.

https://p.dw.com/p/3p35X
Kenia Nairobi | Präsident Somalia | Mohamed Abdullahi Mohamed
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Hii ni baada ya hatamu yake kumalizika leo bila ya makubaliano ya kisiasa kuhusu kura ya kumchagua mrithi wake.

Taifa hilo la Pembe ya Afrika lilipaswa kufanya uchaguzi wake mkuu leo Februari 8, lakini hilo halikufanyika kufuatia mvutano kati ya serikali kuu na majimbo kukosa kukubaliana kuhusu jinsi ya kuendelea mbele na uchaguzi.

Hatua ya kutofanya uchaguzi imeiweka Somalia katika hali tete kisiasa, mnamo wakati nchi hiyo inakabiliwa na ongezeko la mashambulizi ya wanamgambo, uvamizi wa nzige na uhaba wa chakula.

Upinzani wamtaka Farmajo kuheshimu katiba

Muungano wa wagombea wa upinzani katika taifa hilo lenye misukosuko, umemuhimiza rais anayefahamika zaidi kwa jina la utani Farmajo, kuheshimu katiba na ahakikishe madaraka yanakabidhiwa kwa amani.

Picha ya maktaba- Mabango ya wagombea urais yaonekanakando ya barabara mjini Mogadishu February 07,2017.
Picha ya maktaba- Mabango ya wagombea urais yaonekanakando ya barabara mjini Mogadishu February 07,2017.Picha: picture-alliance/abaca/S. Mohamed

Kwenye taarifa yao waliyoitoa usiku wa kuamkia leo, Baraza hilo la wagombea wa upinzani limesema halimtambui tena Farmajo kama rais, kuanzia Februari 8, 2021, na kwamba  halitakubali shinikizo ya aina yoyote ya kurefusha muda wake kama rais.

Kundi hilo limeungana dhidi ya Farmajo lakini lina wagombea binafsi wanaotaka kuwa rais, wakiwemo marais wawili wa zamani wa nchi hiyo.

Wito watolewa wa kuundwa baraza la mpito

Wametoa wito wa kuundwa baraza la mpito la kitaifa, linalowajumuisha maspika wa bunge, viongozi wa upinzani, viongozi wa kidini pamoja na makundi ya wanaharakati, kuliongoza taifa hilo katika kipindi hiki.

Mapema leo, baadhi ya barabara mjini Mogadishu ikiwemo inayoelekea katika bunge zilifungwa, baada ya usiku uliojaa taharuki katika mji huo mkuu. Hayo yamesemwa na mashuhuda walioongeza kuwa hawakuweza kupata usingizi kama kawaida. Abdullahi Ali ambaye ni mmoja wa walioshuhudia ameeleza kwamba wafuasi wa upinzani walikuwa wakifyatua risasi.

Picha ya Maktaba- Watu wakipiga foleni kushiriki uchaguzi wa rais Novemba 13, 2017 Somaliland.
Picha ya Maktaba- Watu wakipiga foleni kushiriki uchaguzi wa rais Novemba 13, 2017 Somaliland.Picha: Getty Images/AFP

Farmajo ambaye anawania muhula wake wa pili anawashutumu wapinzani wake kwa kutotekeleza makubaliano ya awali ya mwezi Septemba, ambayo yaliainisha tarehe ya uchaguzi.

Mzozo kati ya Farmajo na majimbo wakwamisha uchaguzi

Kulingana na makubaliano hayo, uchaguzi wa bunge ungefanyika mwezi Desemba mwaka 2020 na wa rais ungefanyika mapema mwaka 2021.

Lakini makubaliano hayo yalivunjika kufuatia mivutano iliyojitokeza kuhusu namna ya kuandaa uchaguzi.

Jubaland, ambalo ni jimbo linazozana na Farmajo na pia moja kati ya majimbo yenye mamlaka yao ya ndani linamshutumu rais kwa kukataa majaribio ya kuafikiana. Siku tatu kabla ya mazungumzo kati ya pande zote husika kukamilika bila ya makubaliano Ijumaa iliyopita.

Jumuiya ya kimataifa yaonya Somalia ipo katika njia isiyotabirika

Mashambulizi ya mara kwa mara yamekuwa yakifanywa na wanamgambo wa Alshabaab katika mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine ya nchi hiyo.
Mashambulizi ya mara kwa mara yamekuwa yakifanywa na wanamgambo wa Alshabaab katika mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine ya nchi hiyo.Picha: Feisal Omar/REUTERS

Umoja wa Mataifa ulishaonya kwamba Somalia iko katika hatari ya kutumbukia katika hali isiyoweza kutabirika, endapo hatamu ya serikali itamalizika bila ya kuwepo makubaliano kuhusu mchakato wa uchaguzi.

Wiki iliyopita, jumuia ya kimataifa inayoiunga mkono serikali, ikiwemo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, zilionya dhidi ya majaribio ya kuandaa uchaguzi usiokamili au mchakato wowote ambao wengi hawajakubaliana kuhusu.

Somalia ilitumbukia katika machafuko mwaka 1991 baada ya jaribio la kupindua utawala wa kijeshi wa aliyekuwa rais wa wakati huo Siad Barre, hatua ambayo ilisababisha miaka mingi ya vita vya kikoo na kuchangia kuibuka kwa kundi la wanamgambo Al-Shabaab ambalo linadhibiti maeneo makubwa ya nchi hiyo ikiwemo mji mkuu.

(AFPE)