1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wa Zimbabwe washinda uchaguzi wa bunge

Charo, Josephat3 Aprili 2008

Matokeo ya uchaguzi wa rais bado yanasubiriwa

https://p.dw.com/p/DZas
Kiongozi wa chama cha MDC Morgan TsvangiraiPicha: AP

Upinzani nchini Zimbabwe umeshinda uchaguzi wa bunge. Kwa mujibu wa matokeo rasmi ya mwisho yaliyotangazwa usiku wa kuamkia leo na tume ya uchaguzi, chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC, kimepata viti 109 dhidi ya viti 97 vilivyoshindwa na chama tawala cha rais Robert Mugabe, ZANU-PF.

Mgombea huru wa wadhifa wa urais, waziri wa zamani wa habari, Jonathan Moyo, amehifadhi kiti chake cha ubunge katika bunge la Zimbabwe lenye idadi ya viti 210.

Matokeo ya uchaguzi wa rais bado hayajatangazwa lakini kiongozi wa chama cha MDC, Morgan Tsvangirai, amedai ushindi dhidi ya rais Mugabe kwa kupata asilimia 50.3 ya kura. Lakini gazeti la serikali la The Herald, limeripoti leo kwamba duru ya pili itahitajika kuamua mshindi.

Msemaji wa chama cha MDC, Tendai Biti, anasema wameshinda uchaguzi wa rais bila ya duru ya pili na wanasubiri ikiwa tume ya uchaguzi itathibitisha kile ambacho vyombo vya habari vya serikali vimekuwa vikiwaandaa Wazimbabwe kukisikia.

Ingawa chama cha ZANU-PF kimepoteza wingi wa viti bungeni kwa mara kwanza tangu uhuru wa Zimbabwe, hali inafanywa kuwa ngumu kutokana na mpasuko ndani ya cha chama upinzani cha MDC huku wabunge 10 wapya waliochaguliwa wakiwa wanachama wa kitengo cha chama hicho kinachopingana na kiongozi wa chama Morgan Tsvangirai.

Wabunge hao wanamuunga mkono kiongozi wa zamani Arthur Mutambara. Wagombea watatu wa ubunge walikufa wakati wa kampeni na uchaguzi katika maeneo yao ya uwakilishi bungeni utafanywa baadaye.

Mawaziri wanane katika serikali ya rais Mugabe wamepoteza viti vyao vya ubunge.