1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wapamba moto Uarabuni kote - Wahariri

Abdu Said Mtullya2 Februari 2011

Wahariri wa magazeti karibu yote, leo (1 Februari 2011) wanazungumzia juu ya matukio ya nchini Misri na katika nchi nyingine za Kiarabu kwa jumla, wakisema kuwa inavyoonekana mabadiliko yanalikumba eneo hili.

https://p.dw.com/p/1091d
Waandamanaji wakisema Mubarak ondoka!Picha: AP

Katika maoni yake, mhariri wa gazeti la Reutlinger-General-Anzeiger anatilia maanani kwamba viongozi katika nchi takriban zote za kiarabu sasa wanagwaya kutokana na matukio ya nchini Misri na Tunisia.

Mhariri huyo anaeleza kuwa nchini Jordan mfalme wa nchi hiyo amefanya mabadiliko ya serikali ikiwa ni njia ya kujaribu kuepusha upinzani. Nchini Algeria wapinzani wa serikali wameanza kuja juu. Nchini Moroko ni suala la muda tu kabla mambo kuripuka, na nchini Sudan tayari hali imeshaanza kuwa ya mvutano baada ya kura ya maoni kufanyika Sudan ya Kusini. Moto unaowaka sasa unaweza kuenea hadi katika Bara Arabu, ingawa watu katika eneo hilo bado wamo mnamo kiwi cha utajiri wa mafuta.

Hata hivyo, mhariri wa gazeti la Lübecker anasema kuwa mabadiliko ya utawala hayafuatiwi na hatua za maandeleo wakati wote. Mhariri huyo anasema mfano ni mabadiliko yaliyotokea katika nchi za Afrika na katika nchi za Ulaya ya Mashariki zilizokuwa chini ya himaya ya kisoviet- Urusi ya zamani. Anasema ikiwa utawala wa kidikteta unaondelolewa, na mahala pake pakachukuliwa na kikundi kingine cha madikteta, hapo, hapatakuwa na ushindi. Kwa hiyo, ni muhimu kwa wapinzani nchini Misri kusimama pamoja dhidi ya rais Mubarak. Kwani hakuna jambo baya kuliko,kutokea vurumai, baada ya wapinzani kufanikiwa.

Katika maoni yake gazeti la Brauschweiger linazungumzia juu ya maslahi ya kisiasa na ya kiuchumi ya nchi za magharibi nchini Misri na linasema kwamba kwa muda wa miaka mingi,nchi za magharibi zimekuwa zinajihadaa zenyewe kwa kuunga mkono utawala wa kidikteta wa Mubarak kwa sababu za kiuchumi na kisiasa. Nchi za magharibi zimekuwa zinamuunga mkono Mubarak kwa kutumia kisingizio cha tishio la wanaitikadi kali wa Kiislamu. Lakini sasa umma waTunisia na Misri unazitaka nchi za magharibi zionyeshe msimamo wao wazi.

Gazeti la Nürnberger linatilia maanani kwamba mapinduzi yanayotokea nchini Misri hayaongozwi na wanaitikadi kali wa kiislamu. Na anauliza jee nchi za magharibi zina ufahamu finyu juu ya Uislamu? Gazeti hilo linajibu swali hilo kwa kueleza kwamba mapambazuko yanayotokea katika nchi za kiarabu hayokuletwa na wanaitikadi kali wa Kiislamu, bali na akina baba, akina mama na vijana kutoka tabaka la kati. Kwani yale mamilioni ya watu waliojitokeza jana kumtaka Mubarak ang'atuke siyo Waislamu?

Mahariri anasema yapasa watu katika nchi za magharibi wawe waangalifu wanapouzungumzia Uislamu. Siyo sawa kutoa hukumu juu ya Uislamu nje ya mahakama na kuunyima haki ya kuwa na uwezo wa kidemokrasia.Gazeti hilo linasema wapo Waislamu wa kuaminika katika nchi za Ulaya na Marekani wanaopambanua baina ya dini na dola!

Mwandishi/Mtullya Abdu/

Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Miraji Othman