1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani washinda Uchaguzi Ugiriki.

Halima Nyanza5 Oktoba 2009

Chama Kikuu cha Upinzani cha Kisosholisti nchini Ugiriki kinachoongozwa na George Papandreou kimeshinda uchaguzi mkuu wa bunge, uliofanyika jana Jumapili nchini humo.

https://p.dw.com/p/Jxoq
Kiongozi wa Chama cha Kisocholisti kilichoshinda uchaguzi nchini Ugiriki George Papandreou.Picha: picture-alliance/ dpa

Ushindi wa chama hicho umekuja baada ya baada ya wapiga kura kuonyesha kutoridhika kwao juu ya serikali iliyopo madarakani ya Kihafidhina inayoongozwa na Costas Karamanlis inavyoshughulikia msukosuko wa kiuchumi na rushwa nchini humo.

Uchaguzi huo mkuu wa jana Jumapili, umeonekana kuwa ni muhimu katika kutekeleza mabadiliko ambayo yanahitajika, katika nchi hhiyo ambayo ni ya pili kwa umasikini katika nchi zinazotumia sarafu ya Yuro barani Ulaya.

Chama cha Kisosholisti cha PASOK kilipata ushindi huo baada ya kupata asilimia 44 ya kura zote zilizopigwa, dhidi ya chama cha Demokrasia mpya kinachoongozwa na Waziri mkuu Costas Karamanlis, kilichopata kura 34.

Costas Karamanlis
Waziri Mkuu wa Ugiriki aliyeshindwa vibaya katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana nchini humo Costas Karamanlis.Picha: dpa

Chama hicho cha Kisosholisti pia kimepata viti 160 katika bunge la nchi hiyo lenye viti 300, huku mpinzania wake akipata viti 93.

Kwa upande wake kiongozi wa chama kilichoibuka mshindi cha Kisosholisti George Papandreou, amesema ujumbe ulikuwa wazi kwamba wapiga kura wametaka mabadiliko.

Kiongozi huyo pia ameelezea nia dhabiti ya kuleta uwazi katika siasa za Ugiriki.

Karamanlis akubali kushindwa:

Waziri Mkuu anayemaliza muda wake mhafidhina Costas Karamanlis amekubali kushindwa na amejiuzulu kama kiongozi wa chama chake cha kihafidhina cha Demokrasia mpya.

Chama tawala cha kihafidhina cha Waziri Mkuu huyo kinaondoka, baada ya kuwa madarakani kwa miaka mitano na nusu.

Baada ya matokeo hayo chama hicho cha Kisosholisti kitakuwa na kazi ya kuimarisha uchumi wa nchi hiyo, pamoja na kupambana na tatizo la idadi kubwa ya watu wasiokuwa na ajira.

Wakati wa kampeni ya uchaguzi, chama cha upinzani PASOK cha Papandreou, kiliahidi mpango wa Euro bilioni 3 kwa azma ya kufufua uchumi, kuanzisha kodi ya matajiri na kuwasaidia masikini.

Hata hivyo, mabingwa wa mambo wanasema kuwa macho na masikio sasa yataelekezwa juu ya kama kiongozi huyo wa Kisosholisti atateua kizazi kipya cha vijana wenye vipaji vya kiuchumi pamoja na wanamazingira kusaidia kuongoza nchi hiyo ama kujali zaidi kizazi cha zamani kisichokata tamaa na usosholisti.

Rais Obama apongeza:

Wakati huohuo, tayari salamu za pongezi zimeanza kutolewa, kufuatia ushindi huo uliopata chama cha Kisosholisti.

Rais Barack Obama wa Mareakani jana alimpigia simu, Waziri Mkuu huyo ajaye wa Ugiriki George Papandreou, kumpongeza kwa ushindi mkubwa alioupata.

Obama in Moskau bei der New Economic School vor Studenten
Rais Barack Obama wa Marekani tayari amempongeza Waziri Mkuu mtarajiwa wa Ugiriki.Picha: AP

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani, Rais Obama amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa Marekani na Ugiriki na kusema kuwa atafanyakazi pamoja na kiongozi huyo mpya.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa)

Mhariri: Sekione Kitojo