1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yapigwa marufuku na WADA

20 Novemba 2015

Urusi itafanya kila iwezalo kuwasaidia wanariadha wake kushiriki katika Olimpiki 2016 wakati nchi hiyo ikiendelea kufanya mageuzi katika operesheni zake za kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu

https://p.dw.com/p/1H9ZS
Weltverband IAAF Leichtathletik Doping Skandal Russland
Picha: picture-alliance/dpa/H. Hanschke

Hatua ya Shirikisho la Kimataifa la Raidha – IAAF kuwafungia wanariadha wa Urusi kushiriki katika mashindano ya kimataifa imesababisha vikwazo vyingine kwa nchi hiyo. Shirika la Kimataifa la Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kuongeza misuli nguvu – WADA limetangaza kuwa Urusi ni miongoni mwa nchi sita ambazo mashirika yake ya kupambana na matumizi ya dawa hizo yamepigwa marufuku kwa kutozingatia sheria zake.

Mwanariadha wa zamani wa Urusi Olga Bogoslovskaya ambaye sasa ni mwandishi wa habari anasema nchi yake itashirikiana na IAAF. "Tunafanyia kazi vitu vingi. Kwanza, tunakubali masharti ya IAAF na mashirika ya kupambana na dawa za kusisimua misuli. Na tumeunda kamati ya kuangalia suala hilo. Wanachama wake sio tu maafisa wa kiserikali kutoka idara ya michezo lakini pia watu wanaofahamika michezoni. Kwa sasa, IAAF imeunda kikundi maalum kutathmini suala la doping katika siku 60 zijazo, na tutashirikiana nacho kwa karibu. Tutafanya juu chini kuwasaidia wanariadha wetu walio safi kushiriki Michezo ya Olimpiki ya 2016".

Urusi itakuwa na fursa ya kurejeshwa mashindanoni mwezi Machi 2016 wakati IAAF inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake ya kwanza katika mkutano wa Baraza la IAAF nchini Wales. Israel, Andorra, Argentina, Bolivia na Ukraine pia ziligundulika kukiuka kanuni za WADA na haziwezi tena kuendesha miradi ya kupambana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli. Brazil, Ufaransa, Ubelgiji, Ugiriki, Mexico na Uhispania pia zinachunguzwa kwa karibu.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/AP/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu