1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Ukraine wakubaliana kusitisha mapigano

Amina Mjahid
10 Desemba 2019

Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky wamekubaliana mikakati kadhaa ya kupunguza mgogoro wa Ukraine lakini hawakupiga hatua kubwa ya kumaliza kabisa mapigano yaliodumu kwa miaka mitano.

https://p.dw.com/p/3UWxe
Ukraine-Gipfel in Paris
Picha: picture-alliance/AP/EPA/ C. Petit

Mwenyeji wa mkutano huo rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel waliongoza mazungumzo hayo yaliodumu saa 8 katika kasri la Elysee mjini Paris, yaliojikita juu ya kusitisha mapigano kati waasi  wanaotaka kujitenga Mashariki mwa Ukraine na vikosi vya Ukraine.

Mazungumzo hayo yalifuatiwa na mazungumzo ya kwanza ya uso kwa uso kati ya Putin na mchekeshaji aliyechaguliwa rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Taarifa ya pamoja ya pande zote nne zilizokuwepo katika mazungumzo hayo imesema kwa pamoja wamekubaliana kusitisha mapigano na kuendelea na hatua ya kuondoa kikamilifu vikosi vya kijeshi katika eneo la mgogoro ifikapo mwezi Machi mwaka 2020.

Makubaliano mengine yaliofikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha kabisa mapigano kabla ya kumalizika mwaka 2019.

Rais Zelensky amesema pia hatua mpya ya ubadilishanaji wa wafungwa kati ya taifa lake na watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi, itafanyika mwishoni mwa mwezi huu huku rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisema mkutano mwengine wa kilele utafanyika baada ya miezi minne ili kuuangalia tena mambo waliokubaliana kuelekea usitishwaji wa mapigano.

Macron asema mkutano ni njia muhimu ya kusitisha mgogoro wa Mashariki mwa Ukraine

Puitn und Selenskyj mit Macron in Paris
Rais wa UKraine Volodymyr Zelenski, rais wa Ufaransa Emmanuei Macron na rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Imago Images/ITAR-TASS/Russian Presidential Press and Information Office/A. Nikolsky

Macron ameutaja mkutano huo kama mafanikio huku akiuelezea mgogoro kama kidonda kilichowazi katika bara la Ulaya.  Kansela wa Ujerumani kwa upande wake amekiri kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanywa lakini tayari ameona dhamira njema ya kutatua maswali magumu katika mgogoro huo.

Rais Vladymir Putin ameongeza kuwa mkutano uliofanyika ni hatua muhimu ya kuelekea kupunga mapigano Mashariki mwa Ukraine. lakini Zelensky kwa upande wake amesema licha ya matokeo mazuri ya mkutano wake wa kwanza na rais wa Urusi, na mkutano wa kwanza kufanyika ndani ya miaka mitatu alihitaji mengi kufikiwa.

Mkutano huu wa kilele unatekeleza makubaliano ya Minsk ya mwaka 2015 yaliotaka kuondolewa kwa silaha katika maeneo ya mpakani, kutaka Ukraine idhibiti mpaka wake, Uhuru mpana zaidi katika maeneo ya Donetsk na Lugansk nchini Ukraine na kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa.

Hata hivyo hapakuwa na makubaliano yoyote juu ya muda maalum wa kufanyika uchaguzi huo huku Ukraine ikishindwa kupata makubaliano mengine makubwa kutoka kwa Urusi na kushindwa kukubaliana pia juu ya udhibiti wa mpaka wake.

Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Haiko Maas amesema viongozi wa Umoja wa ulaya wataongeza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi. Maas amesema haoni sababu ya kulegeza vikwazo hivyo vilivyowekewa urusi kutokana na jukumu lake la kuuingilia mgogoro wa Ukraine.

Vyanzo: afp, reuters, afp