1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yajipanga kama mpatanishi wa amani Syria

Yusra Buwayhid
7 Februari 2018

Wakati Urusi ikiwa inaedelea kuwa mshirika mwenye nguvu katika vita vya Syria, ikitumia uwezo wake wa kijeshi kumuimarisha Rais Bashar al-Assad, pia inaipa umuhimu zaidi hatua ya mwisho wa vita hivyo.

https://p.dw.com/p/2sEFr
Syrien Putin ordnet Rückzug an - Besuch auf Militärbasis
Picha: picture alliance/ dpa/TASS/M. Klimentyev

Rais wa Syria Bashar Al-Assad amepata nguvu kutokana na mazungumzo ya amani ya wiki iliyopita katika mji wa mapumziko wa Sochi ulioko karibu na Bahari Nyeusi, huku wapinzani wake wakiwa wamedhoofishwa kwa nguvu ya mshirika wake mkuu Urusi. Lakini mshindi mkubwa zaidi inaonekana kuwa ni huyo mshirika wake, yaani Urusi, ambayo kwa sasa imejitwika jukumu la kuongoza sera ya Syria.

Urusi imesema kwamba inajiondoa katika mapambano na badala yake sasa inataka kuwa mpatanishi wa kuleta amani nchini humo. Hatua hiyo ni muhimu kwa nchi ambayo inataka kuondokana na malalamiko inayokabiliana nayo kuhusu Syria, kama ilivyotokea nchini Afghanistan kabla ya Urusi kuondoka mwaka 1989.

Vitaly Naumkin mtaalamu wa sera ya kigeni  ya Urusi amesema kwamba Urusi haijiangalii kama mshirika katika mgogoro huo. Amesema kwamba nafasi ya Urusi ilikuwa ni katika kuisaidia Syria kupambanana ugaidi. Na hilo lishakamilika. Sasa jeshi la Urusi linafanya kazi nyingine, kama vile kutoa misaada ya kiutu, na ujenzi upya wa taifa ameongeza Naumkin, mkurugenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Mashariki katika Chuo cha Kirusi cha Sayansi.

Urusi itaendelea kuwa na kambi zake pamoja na wanajeshi nchini Syria, lakini imetangaza wiki za hivi karibuni kwamba itaondoa wengi wa wanajeshi wake waliopelekwa nchini humo mwaka 2015 kulisaidia jeshi ya Syria. Urusi pia imekuwa ikishirikiana na Uturuki pamoja na Iran kusitisha mapigano katika maeneo mbalimbali nchini kote.

Alexander Lavrentiev, mjumbe maalum wa Putin nchini Syria, amewaambia waandishi habari mwishoni mwa mazungumzo ya amani ya mjini Sochi, kwamba Urusi imeangamiza chimbuko la ugaidi wa kimataifa huko nchini Syria.

Syrien Kämpfe um Rakka
Mapigano yanaendelea nchini Syria kati ya jeshi na waasi.Picha: Reuters/Z. Bensemra

Gonul Tol, mtaalamu katika Taasisi ya Mashariki ya Kati amesema kwamba Urusi sasa ndiyo yenye nguvu ya kufanya maamuzi. Ulimwengu wa Magharibi hauna kweli uwezo wa kuleta utulivu Syria. Hata hivyo, wakati Al-Assad akiwa anapata nguvu, wasiwasi umetanda juu ya uwezo wa Urusi wa kumdhibiti kiongozi huyo.

Mapigano yaendelea Syria

Wakati mazungumzo ya Sochi yakiendelea, mapigano nchini Syra baina ya waasi na vikosi vya serikali pia yakiendelea. Watu kadhaa waliuawa, na hospitali kuharibiwa kwa mabomu, ikiwa ni pamoja na wakati wa mashambulizi ya anga yaliofanywa ama na vikosi vya Syria au vikosi vya Urusi.

Ghanem Balanche, Mkuu wa shirika la usaidizi wa matibabu nchini Syria UOSSM amesema kwa miaka sasa mamia ya hospitali na vituo vya matibabu vimepigwa mabomu huku jumuiya ya kimataifa ikilipa kisogo tataizo hilo.

Fabrice Balance kutoka Taasisi ya Washington amezungumzia zaidi hali ya upinzani wa nchini Syria, ambao unapoteza vyanzo vya fedha na washirika muhimu.

Tol amesema Urusi inatarajia kudhoofisha upinzani nchini Syria. Inautaka upoteze nguvu ili ufanye makubaliano na serikali.

Wakurdi wa magharibi mwa Syria huenda nao wakaegemea upande wa Urusi . Wakati huo huo, sera ya Marekani katika eneo linalodhibitiwa na Wakurdi la kaskazini-mashariki inakosolewa, huku vita dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS vikiwa vinakaribia kumalizika. Marekani inaepuka kuchukua juhudi zozote za kulijenga eneo hilo, huku wakaazi wake wakiwa katika hali ya umasikini na mazingira mabaya yaliotokona na vita.

Hilo linaweza kupelekea Wasyria wa eneo hilo kumuunga mkono Assad, ambaye kwa msaada wa Urusi amewapa ahadi nzuri zaidi hata kama hilo halitosaidia kupatikana uhuru wa kidemokrasia.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae

Mhariri: Sekione Kitojo