1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasalimu amri mbele ya Uruguay

Bruce Amani
25 Juni 2018

Uruguay imechukua  usukani wa  kundi A  na  kumaliza  wakiwa katika  nafasi  ya  kwanza  baada  ya  kuwakandika  wenyeji  Urusi kwa  mabao 3-0.

https://p.dw.com/p/30Frj
Russland WM 2018 l Uruguay vs Russland 3:0 - Spielende
Picha: Reuters/D. Gray

Urusi ambayo  ilianza  vizuri  mashindano  haya  ya  kombe  la  dunia wakiwa  wenyeji  wa  mashindano  haya, walishindwa  kuhimili vishindo  vya  Uruguay  kutoka Amerika ya  kusini  kwa  kukubali kipigo  cha  mabao 3-0 na  kuridhika  na  nafasi  ya  pili  kutoka katika  kundi A. Urusi , ambayo  imekwisha  fuzu  kucheza  katika duru  ya  timu 16 za  mtoano  pamoja  na  Uruguay , baada  ya kushinda  michezo  yake  miwili  ya  mwanzo ilicheza  muda  mwingi wa  mchezo  huo wakiwa  na  watu  10 uwanjani  baada  ya  Igor Smolnikov  kutolewa  kwa  kadi  ya  pili  ya  njano baada   ya  dakika 36. mabao  ya  Luis Suarez, bao  la  la  kujifunga  wenyewe  la Denis Cheryshev  na  bao  la  dakika  za  mwisho  la   Edinson Cavani  yaliwahakikishia  Uruguay ushindi  wa  kwanza  katika  kundi hilo A.

Suarez alifungua  kitabu  cha  mabao  kwa  Uruguay  katika  dakika ya  10  ya  mchezo akifunga  bao  lake  la  saba  katika  kombe  la dunia  na ushindi  wa Uruguay  uliongezeka  pale Diego Laxalt alipopiga  shuti  katika  dakika  ya  23  na  kumgonga  Cheryshev na kujaa wavuni.

Russland WM 2018 l Saudi Arabien vs Ägypten 2:1 Spielende
Salah na wenzake hawakushinda mechi hata mojaPicha: Reuters/D. Staples

Na  mjini  Volgograd , saudi Arabia  iliishinda  Misri  kwa  mabao 2-1 katika  mchezo  ambao  ulikuwa  ni  wa  kutimiza  wajibu.  Salman Al-Faraj alipiga  mkwaju  wa  penalti  kwa  upande  wa  Saudi  Arabia katika  mchezo  mwingine  wa  kundi A dhidi  ya  Misri, na  ulikuwa mchezo  wa  18  wa  kombe  la  dunia  na  ulikuwa  sawa  na  idadi ya  mashindano  ya  kombe  la  dunia  mwaka  2002 yaliyofanyika Japan na  Korea  kusini. Katika  mashindano  yaliyofanyika  nchini Brazil  miaka  minne  iliyopita , kulikuwa  na  mikwaju 13  ya  penalti katika  mashindano  yote.

Matumizi  ya  vidio kuwasaidia  waamuzi  VAR yamechangia  kwa kiasi  kikubwa  ongezeko  la  penalti, na  mfumo  huo  ulitumika  tena kumzawadia  Al-faraj  mkwaju  wa  penalti. Penalti  hiyo iliyopigwa  na Al-Faraj ni  ya  pili  katika  mchezo  huo.

Fahad Al-Muwallad  alipewa  mkwaju  wa  penalti  baada  ya kuchezewa  vibaya  ndani  ya  box  katika   dakika  ya  39 lakini juhudi  zake  hazikuzaa  matunda.

Kwa  upande  wa  Misri , Mohamed Salah  alipachika  bao katika dakika  ya  22  na Salman Al-Faraj  alisawazisha  bao  hilo kabla  ya kipindi  cha  kwanza  kumalizika. Baada  ya  hapo  Saudi Arabia walifanikiwa  kupata  ushindi  muhimu  na  kumaliza  kundi  hilo wakiwa  katika  nafasi  ya  tatu , ba ada  ya  salem Al-Dawsari kufunga  bao  katika  dakika  ya  95.

Mwandishi:  Sekione  Kitojo / rtre
Mhariri: Bruce Amani