1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yazikatia gesi Poland, Bulgaria, EU yasema imejipanga

Daniel Gakuba
27 Aprili 2022

Viongozi wa Ulaya wanajadili mipango ya dharura baada ya Urusi kuzikatia ugavi wa gesi Poland na Bulgaria. Urusi pia yadai kuiharibu shehena kubwa ya silaha ambazo Ukraine ilipatiwa na nchi za magharibi.

https://p.dw.com/p/4AUwd
Polen | Gasverteilanlage in Gustorzyn
Picha: Wojciech Kardas/Agencja Gazeta/REUTERS

Kampuni kubwa ya gesi ya Urusi, Gazprom imesema imeyafunga mabomba ya kusafirisha gesi kwenda Poland na Bulgaria kwa sababu nchi hizo zimeshindwa kulipia huduma hiyo kwa sarafu ya Ruble ya Urusi, kama ilivyoamuliwa na Rais Vladimiri Putin.

Gazprom imesema haikupokea malipo yoyote kutoka nchi hizo tangu mwanzoni mwa Aprili. Kufuatia tangazo hilo la Urusi bei ya gesi imepanda kwa kasi, tukio ambalo rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya amesema ni jaribio la Urusi kuutisha umoja huo.

Soma zaidi: Urusi: NATO yaandaa mazingira ya Vita vya Tatu vya Dunia

Ama katika juhudi za nadra za kidiplomasia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameafikiana na rais wa Urusi Vladimir Putin, kuwa kimsingi Umoja wa Mataifa na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu wanapaswa kuhusika katika kuwaondoa raia walionaswa katika eneo la kiwanda cha chuma katika mji wa Mariupol ulio kusini mashariki mwa Ukraine.

Bildkombo | Vor Treffen Guterres und Putin
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres (kulia) aliitembelea Moscow na kuzungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin na kuhimiza usitishaji wa vitaPicha: Sputnik/UN/dpa/picture alliance

Guterres ataka njia salama kuwaondoa raia maeneo ya mapigano

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema viongozi hao wameyatangaza hayo wakati walipokutana ana kwa ana mjini Moscow.

Akizungumza pia mji Moscow katika mkutano na waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alikuwa amehimiza njia salama kwa raia wa Ukraine wanaotaka kuondoka katika sehemu zenye mapigano.

''Tunahitaji haraka iwezekanavyo, njia za kibinadamu ambazo usalama wake ni wa kuaminika, na unaheshimiwa na wote, kuwaondoa raia na kuingiza msaada kwa mahitaji ya dharura,'' alisema Guterres.

Na kwenye uwanja wa vita, wasiwasi umetanda kuwa mapigano yanaweza kuenea nje ya mipaka ya Ukraine. Kwa siku ya pili mfululizo, milipuko imelitikisa jimbo la Trans-Dniester nchini Moldova, linalothibitiwa na waasi wanaotaka kujitenga.

Ukraine-Kieg | Flüchtlinge aus Mariupol sind in Saporischschja angekommen
Njia salama kwa raia wanaotaka kuondoka katika maeneo ya mivutano ni suala tete katika mzozo huu wa uvamizi wa Urusi dhidi ya UkrainePicha: Leo Correa/AP Photo/picture alliance

Hakuna aliyekiri kuhusika na miripuko hiyo iliyoharibu minara miwili mikubwa ya mawasiliano ya redio, lakini Ukraine imeshutumu Urusi kwa shambulio hilo.

Urusi yadai kuharibu silaha zilizotolewa na nchi za magharibi kwa Ukraine

Urusi kupitia wizara yake ya ulinzi imesema imeharibu shehena kubwa ya silaha ambazo jeshi laUkraine lilizipokea kutoka Marekani na nchi za Ulaya, ambazo zilikuwa zikihifadhiwa katika depo iliyopo kwenye mkoa wa Zaporizhzhia. Haikusema ni aina gani ya silaha ilizoziharibu, katika shambulizi lake hilo la kutumia kombora la masafa marefu.

Soma zaidi:Ujerumani kuisaidia Moldova kukabiliana na wakimbizi 

Kwingineko, makombora ya Urusi yameliharibu daraja kwenye reli muhimu inayounganisha mji wa Odesa kusini mashariki mwa Ukraine na nchi jirani ya Romania, ambayo ni mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO, taarifa hii pia ikiwa ni kwa mujibu wa Ukraine.

Ndani ya Urusi yenyewe, moto umewaka katika ghala la silaha kwenye mkoa wa Belgorod, baada ya kusikika miripuko kadhaa. Gavana wa jimbo hilo Vyacheslav Gladkov amethibitisha tukio hilo kupitia mtandao wa Telegram.

Ujerumani, ambayo ilikuwa imekabiliwa na mbinyo mkali baada ya kukataa maombi ya Ukraine ya kupeleka silaha nzito, imetangaza kuwa itapeleka vifaru vya kupambana na mashambulizi ya ndege za kijeshi.

 

ape, rtre