1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usafirishaji silaha duniani waongezeka - SIPRI

Josephat Charo22 Februari 2016

Usafirishaji wa silaha duniani umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, huku Marekani ikiendelea kuongoza katika biashara hiyo ikifuatiwa na Urusi kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Amani (SIPRI).

https://p.dw.com/p/1Hzf4
Miongoni mwa silaha zinazotengenezwa kwenye mataifa tajiri kama Marekani na kupelekwa kwenye mataifa masikini kama Sudan.
Miongoni mwa silaha zinazotengenezwa kwenye mataifa tajiri kama Marekani na kupelekwa kwenye mataifa masikini kama Sudan.Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Ripoti ya utafiti mpya wa taasisi hiyo yenye makao yake mjini Stockholm, Sweden, inasema silaha zilizopelekwa barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati zimeongezeka.

Zaidi ya nusu ya silaha zilizouzwa Afrika zililetwa na nchi mbili tu; Morocco na Algeria, ambazo zimeingia katika mashindano makali ya uuzaji silaha kati yao. Kwa ujumla licha ya mizozo inayozikabili, nchi za kusini mwa jangwa la Sahara si soko kubwa sana la silaha nzito kwa sababu ya uchumi unaosuasua.

Ripoti hiyo pia inasema kiwango cha silaha kubwa zilizosafirishwa, zikiwemo zile zilizouzwa na zilizotolewa kama michango, kilikuwa asilimia 14 zaidi katika kipindi cha kati ya 2011 na 2015, ikilinganishwa na miaka mitano kabla, huku Marekani na Urusi zikisafirisha silaha nyingi.

Nchi zilizoagiza silaha kwa wingi ni India, Saudi Arabia, China na Falme za Kiarabu. Waandaaji wa ripoti hiyo waliumulika hasa mzozo wa Yemen, ambako muungano unaoongozwa na Saudi Arabia unaiunga mkono serikali kupambana dhidi ya waasi wa Kishia wa Houthi.

Pieter Wezeman, mtafiti mwandamizi wa tasisi ya SIPRI, alisema katika ripoti hiyo kuwa muungano wa nchi za Kiarabu unatumia kwa kiwango kikubwa silaha nzito za kisasa kutoka Marekani na Ulaya nchini Yemen.

Wezeman ameongeza kusema licha ya bei ya chini ya mafuta, shehena kubwa za silaha kuelekea Mashariki ya Kati zimepangwa kuendelea kupelekwa kama sehemu ya mikataba iliyosainiwa miaka mitano iliyopita.

Ripoti hiyo imesema Marekani imeuza au kutoa msaada ya silaha kubwa kwa wateja tofauti tofauti ulimwenguni. "Kadri mizozo ya kikanda inavyoendelea kuongezeka, Marekani inabakia kuongoza kama muuzaji wa silaha duniani kwa kiwango kikubwa," alisema Aude Fleurant, mkurugenzi wa Programu ya Silaha na matumizi ya kijeshi ya taasisi ya SIPRI.

Jadweli ikionesha mgao wa usafirishaji silaha duniani.
Jadweli ikionesha mgao wa usafirishaji silaha duniani.

China na Urusi nazo zaongeza usafirishaji silaha

Mkurugenzi huyo aidha alisema, " Marekani imeuza au kutoa mchango wa silaha kubwa kwa mataifa yapatayo 96 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na sekta ya silaha ya Marekani ina maagizo ambayo bado hayajashughulikiwa, zikiwemo ndege zaidi ya 600 za kivita chapa F-35.

Urusi inabakia katika nafasi ya pili katika orodha ya SIPRI, huku silaha ilizouza zikiongezeka kwa pointi tatu kufikia asilimia 25, ingawa viwango vilishuka mwaka 2014 na 2015 - sambamba na vikwazo vya mataifa ya magharibi dhidi ya Urusi kuhusiana na mzozo wa Ukraine.

India ilinunua idadi kubwa ya silaha za Urusi na SIPRI imewaorodhesha waasi wa Ukraine kuwa miongoni mwa wateja.

Huku silaha zilizosafirishwa barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati zikiongezeka kati ya 2006-2010 na 2011-2015, kiwango cha silaha zilizouzwa Ulaya kilipungua kwa kiwango kikubwa, na zile zilizopelekwa Amerika zikapungua kwa kiwango kidogo, kwa mujibu wa taasisi ya SIPRI.

China ilizipiku Ufaransa na Ujerumani katika miaka mitano iliyopita na kuwa nchi ya tatu inayouza silaha kwa wingi duniani, huku mauzo yake ya nje yakiongezeka kwa asilimia 88. Silaha nyingi za China ziliuzwa katika mataifa mengine ya Asia, huku Pakistan ikiwa mteja mkubwa. Taasisi ya SIPRI imesema China imejijengea uwezo wa kutengeneza silaha za kisasa na haitegemei sana uagizaji wa silaha kutoka nje.

India inabakia kuwa muagizaji mkubwa wa silaha kubwa, ikiagiza asilimia 14 ya silaha zote, ikiwa ni mara mbili ya kiwango inachoagiza Saudi Arabia inayoshikilia nafasi ya pili katika orodha ya nchi zinazoagiza silaha, na mara tatu ya zile zinazoagizwa na China.

Mwandishi: Josephat Charo/afpe/dpae
Mhariri: Daniel Gakuba