1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uso wa Mugabe waingia nuru baada ya kujiuzulu

Oumilkheir Hamidou
26 Novemba 2017

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe alilia na kusikitika akisema "maluteni wake wamemsaliti" alipokubali kujiuzulu wiki iliyopita baada ya miaka 37 madarakani. Hayo ni kwa mujibu wa gazeti la Standard toleo la leo

https://p.dw.com/p/2oHRy
Simbabwe Unterstützer des neuen Präsidenten Emmerson Mnangagwa
Picha: Reuters/M. Hutchings

Rais Emmerson Mnangagwa, ambae zamani alikuwa mtiifu kwa Mugabe, ameapishwa ijumaa iliyopita na walimwengu wanajiuliza kama ataunda serikali ya mchanganyiko wa wafuasi wa vyama tofauti au kama atawateuwa watu wa enzi za Mugabe.

Gazeti la Standard limenukuu duru za karibu sana na Mugabe zikisema muumini huyo wa kikatoliki alikuwa na tasbihi mkononi alipowaambia washirika wake wa karibu pamoja pia na kundi la wapatanishi katika nyumba yake "Blue House" mjini Harare kwamba anajiuzulu. Ametangaza uamuzi huo wakati bunge lilipokuwa likijadili mswaada wa kumpokonya wadhifa wake wa rais.

"Aliangalia chini na kusema "watu wamegeuka kinyonga",mojawapo ya duru hizo imenukuliwa ikisema.

Wazimbabwe washangiria kung'olewa madarakanmi Robert Mugabe
Wazimbabwe washangiria kung'olewa madarakanmi Robert MugabePicha: Reuters/P. Bulawayo

Gazeti linalomilikiwa na serikali Sunday Mail limemnukuu padri Fidelis Mukonori, kasisi mkuu wa madhehebu ya Jesuit, rafiki mkubwa wa Mugabe na ambae ndie aliyepatanisha mvutano  wa kujiuzulu kati ya jeshi na Mugabe, akisema "uso wa Mugabe uling'ara" mara tu baada ya kusaini waraka wa kujiuzulu.

"Kwa hivyo hatuzungumzii kuhusu mtu aliyejaa kinyongo. Nikamwambia ni bora kwake kwamba sasa mtu mwengine anashika hatamu za uongozi wa nchi"  Mukori ameliambia gazeti la Sunday Mail.

Hakuna yeyote, si padri Fidelis Mukori na wala si wasaidizi wa karibu wa Mugabre aliyepatikana kuthibitisha au kukanusha habari hizo.

Kinyang'anyiro cha kuania madaraka kati ya mke wa Mugabe , Grace na msaidizi wake tiifu wa miaka mingi, Emmerson Mnangagwa ndio sababu ya kuangushwa Robert Mugabe.

Gazeti la kibinafsi Standard ambalo daima lilikuwa likimkosoa Mugabe na serikali yake, limemhimiza Mnangagwa, ahakikishe matamshi yake yanafuatiwa na vitendo.

Rais mpya Emmerson Mnangagwa alipokuwa anaapishwa mjini Harare
Rais mpya Emmerson Mnangagwa alipokuwa anaapishwa mjini HararePicha: Reuters/M. Hutchings

Rais mpya Mnangagwa aahidi kuheshimu mfumo wa kidemokrasi na kupambana na rushwa

Katika sherehe za kuapishwa ijumaa iliyopita, Mnangagwa alisema anathamini demokrasia, uvumilivu na utawala unaoheshimu sheria na kwamba atapambana na visa vya rushwa. Amewatolea wito wananchi pia wasilipize kisasi.

Serikali mpaya imeshaanza kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya wafuasi wa Mugabe na mkewe; waziri wa fedha Ignasius Chombo amefikishwa mahakamani jana kwa madai ya rushwa. Chombo ni miongoni mwa kundi la watu wanaoshirikiana na Grace na ambao waliwekwa kizuwizini na kufukuzwa toka chama tawala cha ZANU-PF baada ya jeshi kutwaa madaraka katika kile kilichotajwa kuwa "Opereshini ya kuwatimua wahalifu wanaomzunguka Mugabe."

Chombo alieiambia korti alichukuliwa kwa nguvu kutoka nyumbani kwake November 15 na watu waliokuwa na silaha na waliovalia sare za kijeshi, ataendelea kushikiliwa hadi maombi yake ya kuachiwa kwa dhamana yatakaposikilizwa kesho jumatatu. Alikamatwa na kutiwa pingu miguuni pamoja na mkuu wa tawi la vijana la ZANU-PF Kudzanai Chipanga.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters

Mhariri: Isaac Gamba