1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti: Mabadiliko ya tabia nchi ni kitisho kikubwa duniani

Sylvia Mwehozi
11 Februari 2019

Utafiti mpya ulioendeshwa katika nchi 26 na matokeo kuchapishwa Jumatatu umebaini kuwa nchi nyingi zinaona mabadiliko ya tabia nchi kuwa kitisho kikubwa cha ulimwengu.

https://p.dw.com/p/3D6yH
Kiribati
Picha: picture-alliance/ZUMA Press/UNICEF/Sokhin

Utafiti huo uliofanywa mwaka jana na kituo cha utafiti cha Pew, ulibaini kuwa nchi 13 kati ya 26 zilizoshiriki utafiti huo zilisema mabadiliko ya tabia nchi ndio hatari kubwa ya dunia. Nchi nane zilisema ugaidi unaotekelezwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS ni kitisho kikubwa, ikiwemo Ufaransa na Italia. Lakini nchi nne ikiwa ni pamoja na Japan, Korea Kusini na Marekani zinaona mashambulizi ya mtandaoni ndio yenye kuleta hofu kubwa.

Wasiwasi kuhusu mpango wa nyukilia wa Korea Kaskazini, uchumi wa dunia, nguvu na ushawishi wa China, vilitazamwa pia lakini havikutajwa kuwa kitisho kikubwa miongoni mwa nchi zilizoshiriki.

Nchi ya Poland yenyewe ilitaja uwezo na ushawsihi wa Urusi kuwa kitisho kikubwa. Watu wengi sasa wanaamini uwezo wa Marekani na ushawishi wake ni hatari ikubwa kwa nchi zao ukilinganisha na tafiti zilizofanywa mwaka 2013 na 2017. Karibu nusu ya Wajerumani walioshiriki wana wasiwasi na nguvu na ushawishi wa Marekani, ikiwa umeongezeka kwa asilimia 30 tangu utafiti wa 2013.

Kumekuwepo na mabadiliko kutoka mwaka 2013 wakati watu zaidi kidogo katika nchi hizi walisema Urusi na China ndizo zilikuwa tishio zaidi ikilinganishwa na Marekani.

Illustration - Computer - Cyberkriminalität
Kompyuta inayoonyesha mfano wa shambulio la mtandaoniPicha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Pia utafiti huo ulibaini kwamba wafuasi wa vyama vya kizalendo vyenye siasa kali za mrengo wa kulia, ikiwemo kile cha AfD au chama mbadala kwa Ujerumani, wao hawana mashaka juu ya mabadiliko ya tabia nchi kama kitisho kikuu.

Mkurugenzi mwandamizi wa kituo hicho Jacob Poushter ameiambia dw kuwa mabadiliko ya tabia nchi yameendelea kuleta athari kwa raia wa Marekani na hata mataifa ya Ulaya.

Pia amegusia tofauti ya usawa wa kijinsia ambapo wanawake kwa ujumla wana wasiwasi zaidi na mpango wa nyukilia wa Korea kasakazini, mabadiliko ya tabia nchi duniani na kundi la IS ukilinganisha na wanaume katika nchi za barani Ulaya na Amerika ya Kaskazini ambazo zilifanyiwa utafiti.

Pia mashambulizi ya mtandaoni ni suala ambalo linazidi kujitokeza katika vichwa vya watu wengi. Hofu imezidi katika nchi nyingi juu ya mashambulizi hayo tangu swali hilo lilipoulizwa mwaka 2017.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa

Mhariri: Grace Patricia Kabogo