1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti wa OECD kuhusu hali ya watoto

2 Septemba 2009

Watoto wanahitaji zaidi ya huduma za afya, kinga dhidi ya umasikini na nafasi sawa katika maisha ili waweze kuwa na maisha ya furaha.Hayo wanasema wataalamu wa OECD- jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo.

https://p.dw.com/p/JNff

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na OECD tarehe mosi Septemba , serikali ya Ujerumani inatumia fedha nyingi kuwahudumia watoto na vijana. Inatoa hadi asilimia 20 zaidi, ikilinganishwa na mataifa mengine. Asilimia 40 ya pesa hizo hutumiwa moja kwa moja kuwahuduma watoto kama vile fedha wanazolipwa wazazi. Lakini nchini Denmark au Sweden ambako wazazi hupata nusu ya fedha zinazolipwa Ujerumani, watoto hawakabiliwi na kitisho kikubwa cha kuishi katika hali ya umasikini na wana nafasi sawa ya kupata elimu.

Sababu kuu ni kwamba katika nchi nyingi kuna vituo vya kuwahudumia watoto vinavyogharimiwa na serikali na hata shule za kushinda siku nzima. Kwa hivyo Monika Queisser,kiongozi wa utafiti wa kwanza kufanywa na OECD kuhusu hali ya watoto anasema, Ujerumani inapaswa kuwekeza zaidi katika sekta hiyo. Wakati huo huo anasema huenda ikawa sasa hali imekuwa bora kwani katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Ujerumani imechukua hatua kama vile kuongeza pesa zinazolipwa kwa wazazi na imetoa kipaumbele kuongeza nafasi katika vituo vya kuwahudumia watoto. Ripoti ya OECD imezingatia tarakimu zilizokusanywa miaka minne iliyopita. Queisser anasema watoto wa Kijerumani wanamiliki computer,vitabu na kadhalika lakini kuna kasoro katika tabaka ya maisha na uwezo wa kupata nafasi sawa upande wa elimu.

"Hatari ya kuwa masikini nchini Ujerumani ingali kubwa sana, hasa katika familia zenye mzazi mmoja. Na hilo ndilo kundi linalopaswa kusaidiwa zaidi."

Ripoti ya OECD inaonyesha kuwa katika orodha ya nchi zilizofanyiwa uchunguzi, zile zenye wakazi wengi kama vile Ujerumani na Marekani zimetokea kati kati au theluthi ya mwisho. Lakini hata hivyo Queisser anasema hakuna uhusiano kati ya ukubwa wa nchi na mafanikio ya sera za kijamii.

"Ukiiangalia nchi kama vile Ufaransa iliyo na vituo vingi vya kuwahudumia watoto, idadi ya akina mama wanaofanya kazi ni kubwa zaidi na wanawake nchini humo huzaa watoto zaidi kuliko Ujerumani. Hiyo hudhihirisha kuwa hata taifa kubwa linaweza kuwahudumia zaidi watoto wake."

Hakuna pepo ya watoto kokote duniani. Katika utafiti uliofanywa na OECD, imedhihirika kwamba huduma za watoto, baadhi ya wakati zinaridhisha na wakati mwingine zina walakin.

Mwandishi: M.Fürstenau /ZPR /P.Martin

Mhariri: M.Abdul-Rahman