1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa kijeshi kumfungulia mashtaka ya uhaini Bazoum

Saumu Mwasimba
14 Agosti 2023

Utawala wa mapinduzi ya kijeshi nchini Niger umesema utamfungulia mashtaka ya kile ilichouita ''uhaini wa kiwango cha juu''pamoja na kuhujumu usalama wa taifa rais waliyemuondowa madarakani Mohamed Bazoum.

https://p.dw.com/p/4V8WD
	
Niger Niamey | Abdourahamane Tiani
Picha: Télé Sahel/AFP

Tangazo hilo lililotolewa Jumapili usiku na msemaji wa jeshi Kanali meja,Amadou Abdramane limesema utawala wa kijeshi umekusanya ushahidi muhimu wa kumshtaki rais Bazoum mbele ya mamlaka zenye uwezo wa kuwajibika kitaifa na kimataifa kujibu mashtaka ya uhaini wa kiwango cha juu.Tangazo hilo la jeshi limekuja saa chache baada ya kuonesha kuwa tayari kwa mazungumzo na nchi za jumuiya ya Ukanda wa Afrika Magharibi kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kikanda unaoongezeka. Watu wa karibu na pamoja na chama chake wamesema,rais Bazoum amekatiwa huduma ya umeme na wameishiwa chakula,japo jana usiku watawala wa kijeshi walikanusha ripoti hizo na kuwashutumu wanasiasa wa nchi za Afrika Magharibi na washirika wao wa kimataifa kwa kuendesha kampeini ya uchochezi kuupaka matope utawala huo wa kijeshi.