1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utekelezwaji wa adhabu ya kifo wapungua ulimwenguni

Bruce Amani
10 Aprili 2019

Ripoti ya kila mwaka ya Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International inaonyesha kuwa hukumu za kifo zilizotekelezwa zimepungua.

https://p.dw.com/p/3GXTc
Gegen die Todesstrafe
Picha: picture-alliance/W. Steinberg

Chiara Sangiorgio, ni wakili anayepinga adhabu ya kifo katika shirika la Amnesty International na anasema kuwa kulikuwa na matukio machache sana ya kutekelezwa hukumu za kifo katika nchi kama vile Iran, Pakistan na Iraq katika mwaka uliopita ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Mafanikio hayo hata hivyo yametiwa doa na tamko la karibuni la Sultan Hassanal Bolkianah kuwa watu ambao wanaopatikana na hatia ya kufanya vitendo vya kishoga au uzinzi nchini Brunei watahukumiwa kifo kwa kupigwa mawe.

Mnamo Desemba mwaka jana, mataifa 121 kati ya 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa yalipiga kura ya kusitishwa adhabu ya kifo. Ni mataifa 35 pekee yaliyopinga muswada huo, huku 32 yakijiepusha kupiga kura. Hatua hiyo ya kutia moyo imelifanya shirika la Amnesty International kutangaza kuwa adhabu ya kifo inakaribia kuondolewa kabisa duniani.

Brunei Sultan Hassanal Bolkiah - Neue Gesetze
Sultan Hassanal Bolkiah wa BruneiPicha: Getty Images/AFP

Mwaka jana, Burkina Faso ilifuta adhabu ya kifo. Gambia imetangaza sheria ya kuzua utekelezwaji wa hukumu ya kifo na inatafakari kuondoa kabisa adhabu ya kifo. Serikali mpya ya Malaysia imesitisha utekelezwaji wa adhabu ya kifo, japo bila kuthibitisha hatua hiyo. Jimbo la Washington nchini Marekani limepitisha uamuzi kuwa adhabu ya kifo ni kinyume cha katika.

AI iligundua kuwa Iran iliwanyonga watu 253 katika mwaka wa 2018 – ikiwa ni Zaidi ya nusu ya idadi ya mwaka wa 2017. Sababu kuu, kwa mujibu wa shirika hilo, ni kuwa sheria iliyofanyiwa marekebisho ya Iran kuhusu dawa za kulevya, kumaanisha kuwa watu sasa lazima wapatikane na dawa nyingi za kulevya ili kuhukumiwa adhabu ya kifo. Nchini Pakistan watu 14 waliamriwa kunyongwa, ukilinganisha na watu 250 walionyongwa mwaka wa 2017.

Hinrichtung Troy Davis Georgia USA Flash-Galerie
Maandamano ya kupinga adhabu ya kifo Georgia, MarekaniPicha: AP

AI kwa mara nyingine inaiorodhesha China kuwa nchi inayotekeleza idadi kubwa ya hukumu ya kifo duniani. Shirika hilo linakadiria kuwa China huwanyonga maelfu ya watu kila mwaka. Idadi kamili hata hivyo haipatikani kwa urahisi kwa sababu China inayafanya matukio hayo kisiri.

Mwaka jana, Saudi Arabia ilitangaza kuwanyonga watu 149, wengine wao kwa kukatwa vichwa hadharani. Taifa hilo la kifalme linasema linachapisha takwimu hizi ili kuwazuia watu wanaopanga kufanya uhalifu.

Wakati huo huo Misri iliwanyonga watu 43 katika mwaka wa 2018 na kuwahukumu kifo watu 717, wengi wao kwa makosa yanayohusiana na machafuko ya kuchochewa kisiasa na ugaidi.

Kwa mujibu wa serikali ya Vietnam, watu 85 walinyongwa mwaka jana nchini humo. Na Japan na Singapore zikawanyonga watu 15 na 13, ikiwa ni idadi kubwa kuliko miaka ya nyuma.

Kulikuwa na nchi nne tu kutoka kusini mwa jangwa la Sahara ambazo zilitekeleza hukumu ya kifo mwaka jana. Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Botswana. Nchi 17 za kiafrika zimeondoa aina hiyo ya adhabu.