1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki kuingiza wakimbizi "ikibidi"

7 Februari 2016

Uturuki imesema iko tayari "iwapo ikibidi " kuwaingiza nchini humo maelfu ya Wasyria wanaokimbia shambulio kuu la serikali ikiiungwa mkono na Urusi katika mji wa Allepo ambapo hali inatajwa kuwa ni mbaya sana.

https://p.dw.com/p/1HrBR
Mkimbizi wa Syria akielekea Uturuki.
Mkimbizi wa Syria akielekea Uturuki.Picha: picture alliance/AP Photo

Maelfu ya watu wakiwemo wanawake na watoto wamekwama katika mpaka wa Uturuki baada ya kuzuka kwa wimbi hilo la wakimbizi liliosababishwa na mapigano makali karibu na mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria wa Allepo.

Rais Recep Tayyip Erdogan amewaambia waandishi wa habari "iwapo watafika kwenye mlango wetu na tukiwa hatuna chaguo jengine ikibidi tutalazimika na tutawaingiza nchini ndugu zetu hao."

Kituo cha mpakani cha Uturuki cha Oncupinar ambacho kinakabiliana na kituo cha mpakani cha Ba al Salama kilioko nchini Syria kimeendelea kufungwa Jumapili kwa maelfu ya wakimbizi waliokusanyika hapo kwa siku ya tatu.

Hali ni mbaya

Wamekuwa wakisubiri kwa hamu kufunguliwa kwa mpaka huo wakati malori ya misaada yakiwasilisha misaada ndani ya Syria.Wakibeba vitu vichache mkononi Wasyria wamepiga milolongo kwenye baridi na mvua katika makambi machafu karibu na mapaka na Uturuki wakisubiri mahema yanayotolewa na mashirika ya misaada.Wengine wameripotiwa kulala kwenye maeneo ya wazi, mashambani na barabarani.

Wakimbizi baina ya mpaka wa Syria na Uturuki.
Wakimbizi baina ya mpaka wa Syria na Uturuki.Picha: Reuters/A. Abdullah

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka lenye kutowa misaada ya matibabu limesema makambi kwa ajili ya watu waliopotezewa makaazi yao kaskazini mwa jimbo la Allepo yameelemewa.

Muskilda Zancada mkuu wa tawi la shirika hilo nchini Syria amesema kile linachokiona shirika lake hilo ni hali mbaya katika kitongoji cha Azaz kutokana na kuendelea kwa mapigano na maelfu ya watu kupoteza makaazi yao.

Amesema bado wanaendelea kutathimini hali hiyo lakini hadi sasa wameona matatizo ya nafasi za kuwaweka watu na ukosefu wa maji ya kutosha pamoja na suala la usafi katika maeneo mengi.

Hospitali tatu zilizokuwa zikipatiwa msaada na shirika hilo zimeshambuliwa kwa mabomu hivi karibuni juu ya kwamba kiwango cha uharibifu hakikuweza kufahamika kwani kutokana na kuwepo kwao katika medani za vita inakuwa vigumu kuzifikia.

Nusu ya Wasyria wapoteza makaazi

Zaidi ya watu 260,000 wamekufa katika vita vya miaka mitano nchini Syria ambavyo vinahusisha makundi mbali mbali ya waasi. Wapiganaji wa itikadi kali wa jihadi , Wakurdi na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na Urusi na Iran.

Mkimbizi wa Syria mpakani mwa Uturuki.
Mkimbizi wa Syria mpakani mwa Uturuki.Picha: Reuters/O. Orsal

Zaidi ya nusu ya watu wa nchi hiyo wamepotezewa makaazi na mamia kwa maelfu wengine wamekuwa wakijaribu kukimbilia Ulaya mara nyengine wakigharamika na maisha yao wakati wakivuka bahari ya Mediterenia.

Umoja wa Ulaya hapo Jumamosi umesema serikali ya Uturuki ina wajibu wa kimataifa kufunguwa mipaka yake kwa wakimbizi hao wakati huo huo ikishinikiza nchi hiyo izuwiye kusaidia wakimbizi hao wasiingie Ulaya.

Mpaka uwazi kwa dharura

Afisa wa serikali ya Uturuki amesema kituo cha mpakani cha Oncupinar kiko wazi kwa hali za dharura.Amesema majeruhi saba wamechukuliwa kupelekwa Uturuki hapo Ijumaa na mmoja Jumamosi kwa ajili ya kufanyiwa matibabu katika hospitali nchini Uturuki.

Hali ilivyo katika mji wa Allepo.
Hali ilivyo katika mji wa Allepo.Picha: Getty Images/AFP/Z. Al-Rifa

Suleyman Tapsiz gavana wa jimbo la mpakani la Uturuki la Kilis amesema hapo Jumamosi kwamba Uturuki ambayo tayari inawahifadhi wakimbizi milioni 2.5 wa Syria inawahudumia wakimbizi wengine 30,000 hadi 35,000 ambao wamekusanyika katika mji wa Syria ulio karibu wa Azaz.

Ameongeza kusema wengine 70,000 yumkini wakakimbilia mpakani iwapo majeshi ya Syria yakisaidiwa na mashambulizi ya anga ya Urusi yataendelea kusonga mbele kuelekea Allepo.

Waasi hatarini kusambaratika

Vikosi vya Syria vikisaidiwa na mashmabulizi mazito ya anga ya Urusi vimekuwa vikikaribia kuingia Allepo ikiwa ni hatua kubwa ya kusonga mbele tokea Urusi ilipoingilia kati hapo mwezi wa Septemba kuisaidia serikali inayoongozwa na Rais Bashar al Assad.

Waasi wa Syria.
Waasi wa Syria.Picha: Reuters/A. Abdullah

Waasi wakuu wa Syria wako hatarini kusambaratika baada ya serikali kuikatisha bararabara yao kuu ya kuwafikishia mahitaji katika mji wa Allepo.

Vikosi vya upinzani na takriban raia 350,000 walioko ndani ya maeneo yanayoshikiliwa na waasi katika mji wa Alleopo wako katika hatari ya kuzingirwa na vikosi vya serikali mbinu waliyoitumia na kusababisha madhara makubwa katika miji iliokuwa ngome za waasi huko nyuma.

Hapo Jumamosi Syria ilijibu vikali kuhusiana na dokezo kwamba Saudi Arabia na Uturuki ambazo zinaunga mkono makundi ya waasi zinaweza kutuma wanajeshi wa nchi kavu nchini humo ambapo imesema wavamizi wowote wale watarudi nchini mwao katika majeneza ya mbao.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Daniel Gakuba