1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uungaji mkono kisiasa wahitajika Ukraine

25 Aprili 2014

Ujerumani yapendekeza safari ya pamoja ya ujumbe wa ngazi ya juu wa Marekani,Umoja Ulaya na Urusi na maafisa wa serikali za mitaa kwa maeneo ya vurugu Ukraine kuonyesha uungaji mkono wa kisiasa wa makubaliano ya Geneva.

https://p.dw.com/p/1BoNf
Wanaharakati wanaotaka kujitenga katika mji wa Sloviansk mashariki mwa Ukraine.
Wanaharakati wanaotaka kujitenga katika mji wa Sloviansk mashariki mwa Ukraine.Picha: DW/R. Goncharenko

Katika baruwa iliyotumwa kwa Shirika la Usalama na Ushirikiano Barani Ulaya (OSCE),waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema makubaliano ya kimataifa yaliofikiwa Geneva kutuliza mzozo wa Ukraine yanahitaji kuonekana hadharani kwamba yanaungwa mkono kisiasa.

Ametowa mfano wa kuungwa mkono huko kuwa kunaweza kudhihirishwa wa ziara ya wawakilishi wa ngazi ya juu wa wahusika wote wakuu wanne katika mzozo huo yaani Ukraine yenyewe,Marekani,Umoja wa Ulaya na Urusi kwa mji mkuu wa Kiev na sehemu za mashariki na magharibi mwa nchi hiyo.

Steinmeier amemtumia baruwa hiyo waziri wa mambo ya nje wa Uswisi Didier Burknaller ambaye nchi yake ndio mwenyekiti wa sasa wa shirika la usalama na ushirikino la Ulaya (OSCE). Dondoo za baruwa hiyo zimechapishwa katika gazeti la leo hii la Ujerumani Sueddeutsche Zeitung ambapo pia zimetumwa Washington, Moscow,Brussels na Kiev.

Steinmeier ameandika katika baruwa hiyo kwamba ni muhimu kufanikisha mabadiliko kwa wananchi wa nchi hiyo yatakayoweza kuonekana wazi wazi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.Picha: picture-alliance/dpa

Urusi yapinga kusukumwa

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema Urusi itashirikiana na mataifa ya magharibi kupunguza hali ya mvutano nchini Ukraine lakini haitakubali madai yanayotolewa na upande mmoja. Kauli ya waziri huyo katika mkutano wake na wanadiplomasia mjini Moscow leo hii ilikuwa ikilenga matamshi yaliyotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ambaye ametishia vikwazo vipya dhidi ya Urusi.

Kerry amesema hapo jana vikwazo ambavyo tayari vimeidhinishwa ni kwa ajili tu ya kutathmini vipi dunia itakavyochukuwa hatua iwapo Urusi itaendelea kuuchochea mzozo huo wa Ukraine badala ya kuupoza kama ilivyoahidi.

Amesema kwamba serikali ya Ukraine imekuwa ikifanya juhudi kwa nia njema kutekeleza makubaliano hayo wakati Urusi ikigoma kuchukuwa hatua yoyote ile madhubuti ya kutekeleza makubaliano hayo.

Vita Vikuu vya Tatu vya Dunia

Waziri Mkuu wa Ukraine Arseny Yatsenyuk amesema leo kwamba Urusi inataka kuanzisha Vita Vikuu vya Tatu vya Dunia kwa kuikalia kwa mabavu Ukraine "kijeshi na kisiasa" na kutibua mzozo ambao utazagaa barani kote Ulaya.

Rais Vladimir Putin wa Urusi akizuru kambi moja ya kijeshi karibu na Moscow.
Rais Vladimir Putin wa Urusi akizuru kambi moja ya kijeshi karibu na Moscow.Picha: EPA/ALEXEY NIKOLSKY / GOVERNMENT PRESS SERVICE

Yatsenyuk ameliambia baraza la mwaziri la mpito katika hotuba iliyotangazwa moja kwa moja hewani kwamba majaribio ya kuanzisha mzozo wa kijeshi nchini Ukraine yatapelekea kuzuka kwa mzozo wa kijeshi barani Ulaya.

Amesema dunia bado haikusahao Vita Vikuu vya Pili vya Dunia,lakini Urusi tayari inataka kuanzisha Vita Vikuu vya Tatu vya Dunia.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman