1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uuzaji wa silaha duniani waongezeka kwa 8%

Grace Kabogo
11 Machi 2019

Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa masuala ya amani duniani SIPRI imesema uuzaji wa silaha za kivita duniani umeongezeka kwa kiasi cha asilimia nane kwa kipindi cha mwaka 2014 hadi 2018 ikilinganishwa na 2009 hadi 2013.

https://p.dw.com/p/3ElcF
Minigun Stand MG Symbolbild Waffenexporte
Picha: picture-alliance/dpa/J. Lo Scalzo

Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa masuala ya amani duniani, SIPRI imesema uuzaji wa silaha za kivita duniani umeongezeka kwa kiasi cha asilimia nane katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2018 ikilinganishwa na 2009 hadi 2013.

Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya SIPRI  iliyotolewa leo, Marekani inaongoza kwa kuuza silaha duniani, ambapo imesafirisha zaidi ya theluthi ya silaha katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Marekani imesafirisha asilimia 36 ya silaha zote zilizouzwa kati ya mwaka 2014 na 2018, hiyo ikiwa ni asilimia sita zaidi ikilinganishwa na mwaka 2009 hadi 2013.

Marekani yauza silaha kwa nchi 98

Taasisi hiyo yenye makao yake mjini Stockholm, Sweden ambayo pia inachunguza uuzaji wa silaha dunia, imesema Marekani imeuza silaha kwa nchi zipatazo 98 duniani, huku nusu yake zikiwa zimeuzwa katika eneo la Mashariki ya Kati. Saudi Arabia, mshirika wa Marekani ilikuwa soko muhimu zaidi kwa silaha za Marekani. Moja kati ya silaha nne za Marekani ziliuzwa Saudia kati ya mwaka 2014 hadi 2018.

F-22 'Raptor' Kampfjet
Moja ya ndege za kivita za MarekaniPicha: picture-alliance/dpa/J. Heon-Kyun

Saudi Arabia pia ilinunua silaha nyingi zaidi ya nchi yoyote ile, sawa na asilimia 12 ya uingizaji wa bidhaa kimataifa, ambapo ilikuwa mteja mkuu wa Marekani, Uingereza na Ufaransa. Urusi imeshika nafasi ya pili kwa kuwa muuzaji wa silaha duniani. Hata hivyo, mauzo ya Urusi yalipungua kwa asilimia 17 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka 2009 hadi 2013 kutokana na India na Venezuela kupunguza uingizaji wa silaha. Zaidi ya nusu ya silaha za Urusi zilikwenda India, China na Algeria.

Nafasi 5 za juu

SIPRI imesema nchi nyingine zilizoshika nafasi tano za juu katika kuuza silaha duniani ni pamoja na Ufaransa, Ujerumani na China, ambazo zilisafirisha tatu kati ya silaha 4 duniani katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2018. Ujerumani iliongeza mauzo yake ya silaha kimataifa kwa asilimia 13, pamoja na manowari za kivita zilizotengenezwa Ujerumani.

Ripoti ya SIPRI imefafanua kuwa aina ya silaha zilizouzwa katika kipindi hicho ni pamoja na ndege za kijeshi, makombora na vifaru, lakini haikuzingatia silaha ndogo ndogo kama vile bunduki. Utafiti wa SIPRI umefanikiwa kutokana na takwimu zilizopatikana kupitia vyanzo kama vile magazeti na taarifa za serikali, ambapo wataalamu walizikusanya katika kila nchi silaha zinaposafirishwa.

Aidha, mtaalamu wa SIPRI, Pieter Wezeman amesema kuwa silaha nyingi zimeuzwa katika Mashariki ya Kati kutokana na kuongezeka kwa mizozo kwenye ukanda huo, hali iliyoyafanya mataifa tajiri kununua silaha kutoka nchi za Magharibi.