1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uwanja Ndege wa Bangkok umefungwa

26 Novemba 2008

Wasafiri hadi 3000 wamenasa-hali ya hatari kutangazwa ?

https://p.dw.com/p/G2H4
Wapinzani wa serikali-Thailand.Picha: AP

Mgogoro nchini Thailand kati ya serikali na Upinzani,umepambamoto.Waandamanaji wameuteka uwanja wa ndege wa kimataifa wa BangKok na maalfu ya watalii wamenasa hawawezi kusafiri.

Baada ya miripuko kadhaa ya mabomu mjini humo na kuzingirwa kwa barabara mbali mbali na waandamanaji,Uwanja wa ndege leo umefungwa .

Mjini Bangkok,mji mkuu wa Thailand, inatarajiwa sana kuwa waziri mkuu Somachai Wongsowat, mara tu akirejea masaa machache kutoka sasa kutoka mkutano wa kilele wa APEC nchini Peru, atatangaza hali ya hatari nchini.Kwa muujibu wa taarifa za vyombo vya habari,mabomu 3 yaliripuka Uwanja wa ndege wa kimataifa na watu kadhaa wamejeruhiwa .Bomu jengine liliripuka katika uwanja wa ndege wa zamani ambao unatumika kwa safari za ndani na ambako serikali ya Thailand imepiga kambi yake ya muda .Sababu ya hatua hii, ni kuwa Jengo kuu la serikali mjini Bangkok tangu miezi kadhaa , limekaliwa na wafuasi wa"Ushirika wa umma kwa demokrasi (PAD)".

Mashirika kadhaa ya ndege yamevunja safari zao kutoka na kuelekea Bangkok.Zaidi ya abiria 10.000 miongoni mwao watalii wa kigeni,wamenasa hawawezi kusafiri.

Mtalii mmoja asema:

"Sielewi safari yangu ilivyo.Hawatupi taarifa i zozote, nimekasirika kweli na nasikitika,kwani, nina watoto wadogo 2 hapa na tuna hamu ya kurejea nyumbani."

Watalii wengine ambao waliweza kusafiri na ndege ya mwisho kutoka Bangkok na kutua Singapore,wameripoti juu ya hali ya mchafuko iliopo Uwanja wa Ndege wa Bangkok.

Mmoja wao asema:

"Tulipokuwa njiani kuelekea Uwanja wa Ndege, tulijionea waandamanaji wametanda n jia nzima.Na upande wapili ulisheheni polisi."

Mtalii mwengine akaongeza:

"Tulikuwa na hofu kubwa.Lakini tulipokwisha wasili Uwanja wa Ndege ,tulipumua na kuhisi tuko salama .Tulikuwa na wasi wasi kwamba, ndege ingekawia kuondoka au isingeruka kabisa,lakini kila kitu kilienda sawa sawa.Tunamshukuru Mungu tumewasili nyumbani."

Karibu na Uwanja wa ndege wa Bangkok "Don Muang" kulizuka mapigano makali hapo jana.Wapinzani wa serikali waliokuwa na silaha waliwafyatulia risasi wafuasi wa serikali.Si chini ya watu 11 walijeruhiwa -hii ni kwa muujibu wa TV ya Thailand ilivyoripoti.

Maalfu ya wafuasi wa Upinzani (PDA) waliofufua kampeni yao hapo Mei mwaka huu baada ya washirika wa waziri mkuu wa zamani Thaksin waliposhinda uchaguzi mwaka jana, wamepiga kambi yao nje ya uwanja wa ndege na wamejieneza ndani ya uwanja huo.

Wakuu wa usafiri wametangaza kwamba, uwanja huo wa ndege utabakia umefungwa hii leo na hii itawazuwia kusafiri abiria hadi 3000 katika uwanja huo mpya wa ndege na wa kisasa kabisa uliojengwa na utawala wa waziri mkuu wa zamani Thaksin.