1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uwekezaji katika sarafu za digitali washika kasi Uganda

Iddi Ssessanga
18 Januari 2018

Wimbi la watu kuwekeza katika sarafu za dijitali limeshika kasi nchini Uganda, licha ya benki kuu nchini humo kutahadharisha umma kuhusu mashaka ya biashara hiyo inayohusisha sarafu maarufu kama vile Bitcoin.

https://p.dw.com/p/2r49F
Bitcoin
Picha: picture-alliance/dpa/J. Kalaene

Wimbi la biashara hii limeshika kasi hasa kutokana na ahadi za kupata utajiri wa ghafla ikiwa mtu atawezekeza katika kununua sarafu hizo kupitia kwenye mitandao.

Wimbi kuwekeza katika sarafu hizo limetandaa kote duniani tangu uvumbuzi wake mwaka 2009. Mbali na Bitcoin kuna sarafu zingine kama onecoin ambayo imeanza kuwa maarufu Uganda, kuna Litecoin, Ethereum, Zcash, Dash na kadhalika.

Kulingana na wale wanaoshiriki biashara hii, yeyote atakaepuuzilia kuwekeza katika sarafu za kidijitali atajuta maishani kwani ndiyo sarafu zitakazotumiwa siku zijazo kote duniani. Jukwaa la benki kuu duniani halijatoa ufafanuzi kuhusu athari za sarafu hizo zinazouzwa mtandaoni bila kuhusisha benki za kibiashara.

Bitcoin
Muonekano wa sarafu halisi ya Bitcoin.Picha: picture-alliance/NurPhoto/M. Romano

Benki Kuu haina uwezo wa kuingilia

Huku baadhi ya nchi kama Urusi zikikubali matumizi waziwazi wa sarafu hizo katika biashara, nchi kama Korea kusini zimetisha kuzipiga marufuku. Benki kuu ya Uganda imetahadharisha umma dhidi ya biashara hiyo, lakini haina uwezo wa kuzuia watu kujiingiza.

Licha ya faida kubwa wanayodai kupata katika muda mfupi, washiriki katika biashara hii hawataki kuzungumzia hasara anayopata mtu wakati thamani ya sarafu inapoporomoka. Kwa mfano katika muda wa wiki mbili tu, sarafu ya Bitcoin ilikuwa imeshuka kutoka dola elfu ishirini hadi kumi.

Kwa mujibu wa maelekezo kwenye mitandao ya kijamii, sambamba na kuwavutia watu kushiriki biashara hii, kuna onyo katika herufi ndogo kwamba bidhaa hizo za kifedha zina mashaka mengi.

Mteja anatahadharishwa kwamba anaweza kupoteza pesa zake zote. Ushauri ni kwamba wekeza tu pesa ambazo hutajutia kupoteza.

Infografik Wechselkurs Bitcoin - Euro DEUTSCH
Mchoro unaoonyesha kiwango cha ubadilishanaji wa sarafu ya Bitcoin dhidi ya euro.

Matarajio ya wawekezaji

Hata hivyo kwa mtazamo mwingine kuna dhana kwamba kuwepo kwa sarafu hizo ni uvumbuzi utakaorahisisha biashara duniani pamoja kuhamisha pesa na utajiri wa mtu kwa wepesi na kwa gharama ndogo ikilinganishwa na sasa. Lakini mashaka ni kwamba ukipata hasara au ukishirikiana na matapeli huna pa kuwasilisha malalamiko.

Kwa sasa biashara hiyo ya bitcoin yaweza kuelezwa kuwa ni mchezo wa  bahati nasibu. Kwa bahati mbaya itakuwa msiba kwa wale wanaouza mali zao ikiwemo ardhi, nyumba na kadhalika kuwekeza katika biashara hii. Iwapo watapata faida, ni majaliwa lakini hakuna hakikisho.

Mwandishi: Lubega Emmanuel - DW, Kampala

Mhariri: Saumu Yusuf