1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vinavyosababishwa na uvutaji sigara vinaongezeka

P.Martin15 Juni 2008

Kutoka zaidi ya wavutaji sigara bilioni 1.3 walio hai hivi sasa,kama milioni 650 watafariki kwa maradhi yanayosababishwa na uvutaji sigara.Hilo ni onyo lililotolewa katika ripoti ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/EK0u
** EMBARGOED UNTIL 2200 GMT WEDNESDAY, FEB. 13, 2008 ** An Indian worker lights a bidi, a small, cheaply made cigarette in Vadodara, India, Wednesday, Feb. 13, 2008. India is in the grips of a smoking epidemic that is likely to cause nearly a million deaths a year by 2010, more than half of them among poor and illiterate people, according to a study released Thursday. (AP Photo/Ajit Solanki)
India ni miongoni mwa nchi ambako idadi ya wavutaji imeongezeka.Picha: AP

Ripoti iliyotayarishwa na tume ya wajumbe 20 kutoka takriban mashirika yote muhimu ya Umoja wa Mataifa na mashirika ndugu inasema,uvutaji sigara hasa unaua watu wanapokuwa katika upeo wa uzazi,kinyume na vifo vinavyotokea kwa sababu nyingi zingine.Idadi ya vifo vya aina hiyo,inatazamiwa kuongezeka hadi milioni 8.3 ifikapo mwaka 2030 na zaidi ya asilimia 80 ya vifo hivyo vitatokea katika nchi zinazoendelea.Inatathminiwa kuwa ifikapo mwaka 2015,asilimia 10 ya maradhi yote duniani,yatasababishwa na uvutaji sigara kulinganishwa na asilimia 2.6 katika mwaka 1990 na yataua watu wengi zaidi kuliko ugonjwa wo wote mwingine.

Kwa mujibu wa Baraza la Uchumi na Jamii-ECOSOC, uvutaji sigara hauathiri vibaya afya,jamii na mazingira tu,bali hata jitahada za Umoja wa Mataifa kupiga vita umasikini.Wakati huo huo,Shirika la Chakula na Kilimo FAO linasema,wakati ambapo uzalishaji wa tumbaku unapunguka katika nchi zilizoendelea,hali ya mambo ni kinyume kabisa katika nchi zinazoendelea.Kwa mfano, katika mwaka 1970,tumbaku iliyotoka nchi zinazoendelea ilikuwa chini ya asilimia 60 ya tumbako yote duniani.Lakini uchunguzi unaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2010 nchi hizo huenda zikazalisha zaidi ya asilimia 80 ya tumbaku duniani.Sababu ni kuwa katika nchi zinazoendelea,gharama za kuzalisha tumbaku ni ndogo na wakati huo huo mahitaji ya zao hilo yanaongezeka katika nchi hizo.

Lakini kuna habari nzuri pia,kwani mwenendo mpya wa watu kudai haki ya kupumua hewa isiyochafuliwa na moshi wa sigara,umesababisha baadhi ya nchi kupitisha sheria zinazopiga marufuku kuvuta sigara katika maeneo fulani.Hata azimio lililopitishwa na ECOSOC Julai 2006,lilitoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzingatia kupiga marufuku uvutaji sigara ndani ya majengo yote ya umoja huo na sio katika baadhi ya ofisi zake tu. Azimio hilo vile vile linasema,biashara yo yote inayohusika na tumbaku,ipigwe marufuku katika majengo yote ya Umoja wa Mataifa. Lakini hakuna hatua iliyochukuliwa na Baraza Kuu.

Ripoti mpya iliyotayarishwa na wajumbe 20,inatoa wito kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuzingatia suala hilo, baraza hilo litakapokutana kwa kikao chake cha 63 Septemba ijayo.Ripoti hiyo mpya itawasilishwa rasmi katika mkutano wa Baraza la Uchumi na Jamii-ECOSOC utakaofanywa Juni 30 hadi Julai 25.