1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo wakati wa kura ya maoni Sudan kusini

11 Januari 2011

Huku kura ya maoni ikiendelea Sudan kusini watu kumi wameuwawa walipokuwa wakirudi kutoka Kaskazini. Na Rwanda inatarajiwa kuongeza wanajeshi wake wa kulinda amani katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/zwP8
Siku ya tatu ya kura ya maoni SudanPicha: AP

Uvamizi dhidi ya raia hao unasemekana kufanywa na wazee wa kikabila wa kiarabu. Wakati huo huo Serikali ya Rwanda inatayarisha kikosi cha wanajeshi zaidi wa kulinda amani watakaotumwa nchini humo.

Rückkehrer gestrandet Südsudan
Raia wengi wanaorudi kutoka KaskaziniPicha: DW

Waziri wa ndani wa Sudan ya kusini, Gier Chuang Aluong amewaambia waandishi wa habari kwamba Wazee wa kabila la Misseriya hapo jana waliuzuia msafara wa mabasi 30 na malori 7 yaliokuwa yakielekea Sudan Kusini kutoka mji wa Khartoum. Watu kumi waliuwawa huku wengine 18 walijeruhiwa katika shambulio hilo katika mpaka wa Kaskazini na kusini.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa mataifa, zaidi ya watu laki moja wamerudi kusini kutoka kaskazini katika miezi ya hivi karibuni ili waweze kuishi katika kile wanachotarajia kuwa taifa huru.

Huku hofu ikiwa imepungua katika miezi ya hivi karibuni ya kuzuka upya vita vikuu wakati Sudan ya kaskazini inaonekana kuwa tayari kukubali kujitenga kwa kusini, Kura hiyo ya maoni imezidisha wasiwasi kati ya Waarabu wa Kimisseriya, kabila la kaskazini linalosafiri katika eneo lililo na utajiri wa mafuta la Abyei kila mwaka, na kabila la Dinka la kusini.

Rwanda kutuma wanajeshi zaidi

Darfur UNAMID
Rwanda ina wanajeshi 3,300 katika ujumbe wa UNAMIDPicha: AP

Wakati hayo yanajiri Serikali ya Rwanda inatayarisha kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani watakaotumwa aidha katika eneo linalokumbwa na mzozo nchini humo Sudan, Darfur, au katika Sudan ya kusini.

Waziri wa ulinzi wa Rwanda James Kabarebe, amesema wanatayarisha kikosi hicho iwapo kitahitajika katika maeneo yoyote kati ya hayo mawili nchini Sudan.

Mwishoni mwa mwezi wa Agosti, baada ya kuchapishwa ripoti ya Umoja wa mataifa kuhusu uhalifu wa kivita unaosemekana kutekelezwa na Rwanda katika jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Rwanda ilitishia kuwaondoa wanajeshi wake katika operesheni zote za kulinda amani, kwa kuanza na Sudan.

Rwanda ina wanajeshi 3,300 katika ujumbe wa pamoja wa Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika jimboni Darfur UNAMID, ambao kwa jumla una wanajeshi 22,000.

Sikiliza mahojiano kati ya Balozi Yusuf Nzibo, kiongozi wa ujumbe wa IGAD ulioko Juba, Sudan kuhusu hali ilivyo nchini humo. Alikuwa akizungumza na Thelma Mwadzaya.

Mwandishi: Maryam Abdalla/AFPE/DPAE
Mhariri: Abdul-Rahman