1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Kikurdi vyaisambaratisha IS Syria

Grace Kabogo
23 Machi 2019

Vikosi vya Kikurdi vinavyopigania demokrasia Syria, SDF vimelisambaratisha kundi la Dola la Kiislamu, IS, kutoka kwenye ngome yao ya mwisho kwenye kijiji cha Baghouz kilichoko mashariki mwa Syria.

https://p.dw.com/p/3FZDQ
Syrien SDF Flagge in Baghouz
Picha: Getty Images/AFP/G. Cacace

Tangazo hilo la vikosi vya SDF vinavyoungwa mkono na Marekani, linahitimisha uwepo wa wapiganaji hao wa jihadi wa IS ambao walijitangazia utawala wa ukhalifa mwaka 2014. Msemaji wa SDF, Mustafa Bali, alitangaza ushindi huo kupitia ukurasa wake wa Twitter, akisema Baghouz imekombolewa. ''Ushindi wa jeshi dhidi ya wapiganaji wa IS umekamilika,'' alisema Bali.

Mkuu wa uhusiano wa mambo ya kigeni wa SDF, Abdel Kareem Umer amesema kwamba hilo ni tukio la kihistoria, lakini ameonya kuwa ushindi huo haumaniishi ndiyo mwisho wa ugaidi au IS. ''Tumelisambaratisha jeshi la IS, tumeumaliza utawala wao. Lakini bado IS ina mizizi na itikadi zao zinaendelea katika maeneo ambayo waliwahi kuyatawala kwa miaka kadhaa,'' alifafanua Umer.

Udhibiti wa IS

Kundi la IS liliwahi kuyadhibiti maeneo makubwa ya Iraq na Syria, ingawa katika harakati za kuyakomboa maeneo hayo, zilizoendeshwa na Marekani na washirika wake kwa muda wa miaka mitano, magaidi wengi na raia waliuawa.

Syrien Zerstörung in Baghus
Eneo la Baghouz, lililokuwa ngome ya mwisho ya ISPicha: Getty Images/C. McGrath

Mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa Syria na Kikurdi, Mutlu Civiroglu, amesema kuna taarifa kwamba mashambulizi ya anga na mapigano bado yanaendelea kwenye kijiji cha Baghouz, licha ya vikosi vya SDF kudai kuwa wamelikomboa eneo hilo kwa asilimia 100.

Kamanda mkuu wa vikosi vya SDF Mazlum Kobane amethibitisha kuwa wapiganaji wa IS wamesambaratishwa kabisa katika ngome yao ya mwisho. Aidha, ameushukuru muungano wa kijeshi wa kimataifa kutokana na mchango wao mkubwa katika kupambana na IS.

Mjumbe wa Marekani katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani katika mapambano dhidi ya IS, William Roebuck amepongeza hatua ya kukombolewa kwa kijiji cha Baghouz, huku akisema huo ni ushindi muhimu sana wa kihistoria.

Mjumbe wa Marekani aonya

Lakini ameonya kuwa mapambano dhidi ya wapiganaji wa jihadi bado hayajamalizika. ''Tumeisambaratisha IS Syria na Iraq, lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya kufikia malengo ya kupambana kabisa na IS kwa asilimia 100,'' alisisitiza Roebuck.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema chanzo cha mashambulizi ya kigaidi kimeondolewa, lakini ameonya kwamba kitisho bado kiko na kwamba pamambano dhidi ya makundi ya kigaidi yanapaswa kuendelea.

Frankreich | Treffen Theresa May mit Emmanuel Macron
Waziri Mkuu Theresa May (kushoto) na Rais Emmanuel Macron Picha: Reuters

Matamshi ya Macron yametolewa wakati ambapo Waziri Mkuu wa Ufransa, Edouard Philippe na maafisa wengine wamekusanyika mjini Trebes, kusini mwa Ufaransa ikiwa ni kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu yalipotokea mauaji yaliyofanywa na mpiganaji anayedaiwa kuwa mwanachana wa IS, katika eneo la maduka huko Trebes.

Ufaransa imekumbwa na mfululizo wa mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na wapiganaji wa jihadi ambayo yamewaua watu 250 tangu mwaka 2015.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May amepongeza hatua ya vikosi vya SDF kuliangusha kundi la IS nchini Syria na ameapa kwamba serikali ya Uingereza itaendelea kujitolea katika kuondoa sumu ya itikadi iliyopandikizwa na IS. Amesema majeshi ya Uingereza yataendelea kushirikiana na washirika wao ambao wanapambana na IS nchini Syria na Iraq.