1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpiganaji mmoja wa Alshabaab auawa

Admin.WagnerD1 Septemba 2015

Wanamgambo wa kundi la Alshabab wameivamia kambi ya jeshi ya vikosi vya kulinda amani vya umoja wa Afrika kusini mwa Somalia mapema hii leo na askari kadhaa wa vikosi hivyo wanadaiwa kuawawa katika shambulizi hilo.

https://p.dw.com/p/1GP9p
Wanajeshi wa umoja wa Afrika wanaolinda amani nchini Somalia
Wanajeshi wa umoja wa Afrika wanaolinda amani nchini SomaliaPicha: picture alliance/AP Photo/Jones

Wanamgambo wa kundi hilo la Alshabab ambao wana mahusiano ya karibu na kundi la Alqaeda wamesema kuwa mmoja wa wapiganaji wake aliekuwa ndani ya gari aliingiza kwa nguvu gari katika kambi hiyo na kujilipua na kufuatiwa na hatua ya wanamgambo hao kuvamia kambi hiyo ya wanajeshi wa vikosi vya kulinda amani vya umoja wa Afrika AMISOM.

Alshabab wamesema jumla ya wanajeshi wa kulinda amani wa Afrika wapatao 50 wameuawa katika shambulizi hilo lililofanyika katika kambi ya Janale iliyoko kilomita 90 kusini mwa mji mkuu wa Somalia Mogadishu.

Kambi ya Janale yadhibitiwa na Al shabaab

Katika siku za nyuma inaarifiwa kundi hilo limewahi kutoa taarifa za kukuza idadi ya wanajeshi waliouawa na maafisa wa vikosi hivyo vya kulinda amani vya Afrika wamekuwa wakikanusha taarifa hizo.

Hivi sasa kambi ya Janale ya AMISOM iko chini ya udhibiti wetu, Msemaji wa wa operesheni za kijeshi wa kundi hilo la Al-shabaab, Sheikh Abdiasis Abu Musab aliliambia shirika la habari la Reuters.

Mmoja wa wanamgambo wa Al shabaab
Mmoja wa wanamgambo wa Al shabaabPicha: picture-alliance/landov

Kapteni Bilow Idow ambae ni afisa wa kijeshi wa Somalia alieko katika mji wa karibu na kambi hiyo ya Janale amesema mawasiliano kwa njia ya barabara katika eneo hilo yamekatika kwa sasa baada ya wanamgambo hao kuharibu daraja lililoko karibu na kambi hiyo. Hakuna msaada unaoweza kutolewa na kufika eneo hilo kwa sasa, kuna vifo vingi na uharibifu mkubwa, alisema afisa huyo.

Hali bado tete Somalia

Maafisa wa vikosi hivyo vya AMISOM pamoja na maafisa wa serikali ya Somalia hawakuweza kupatikana kwa ajili ya kuzuingumzia shambulizi hilo lakini wakazi jirani na eneo hilo wamethibitisha kutokea kwa shambulizi hilo.

"Baada ya sala ya asubuhi tulisikia mlipuko mkubwa uliofuatiwa na milio ya risasi kutoka katika kambi hiyo ya AMISOM. Hatuna taarifa zaidi kwa vile tuko ndani," alisema mkazi mmoja aliefahamika kwa jina la Ahmed Olow.

Kundi la wanamgambo hao wa Alshabab ambao wanataka kuiangusha serikali ya Somalia inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi ili kulazimisha kuingiza tafsiri yake kuhusiana na imani ya kiisilamu nchini Somalia limekwisha fanya mashambulizi kadhaa katika mataifa ya jirani kama vile Kenya na Uganda kama njia ya kulipiza kisasi dhidi ya hatua ya kupelekwa kwa vikosi vya kulinda amani vya umoja wa Afrika.

Mwandishi: Isaac Gamba/RTRE/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman