1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wakemea kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi

Grace Kabogo
23 Januari 2020

Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence amewataka viongozi duniani kuhakikisha kwamba mauaji mengine ya Wayahudi hayatokei tena na ametoa wito wa kuungana dhidi ya Iran.

https://p.dw.com/p/3WiZ6
Israel World Holocaust Forum Bundespräsident Frank-Walter Steinmeier
Picha: picture-alliance/dpa

Kauli hiyo ameitoa leo katika kongamano la kumbukumbu mauaji dhidi ya Wayahudi mjini Jerusalem, Israel.

Akizungumza mbele ya kiasi ya viongozi wa nchi 50 katika kongamano linalofanyika kwenye kituo cha kumbukumbu ya mauji ya Wayahudi cha Yad Vashem, Pence amesema leo wanakumbuka kilichotokea wakati watu wasio na sauti walipolia kuomba msaada na waliokuwa na uwezo wa kuwasaidia hawakufanya hivyo.

Amesema wanapaswa kujiandaa kuwakabili na kuwafichua wale wanaoeneza chuki na ghasia dhidi ya Wayahudi, ambayo inachochea vurugu ulimwenguni kote. Pence ameutaka ulimwengu kusimama pamoja na kuikosoa vikali Iran, kwani serikali ya nchi hiyo imekuwa ikikanusha kuhusu mauaji ya Wayahudi. Iran imekuwa ikipinga kuhusu mauaji hayo kama suala la sera ya serikali na imetishia kulifuta taifa la Israel katika ramani ya dunia.

''Kwa viongozi wote na mataifa yote ambayo tumekusanyika hapa, leo tuna jukumu na mamlaka ya kuhakikisha kwamba tunachokikumbuka hapa leo, hakijirudii tena,'' alifafanua Pence.

Kwa upande wake Rais wa Urusi Vladmir Putin amesema mauaji ya Wayahudi ni moja kati ya wakati mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mwanadamu. Akihutubia katika kongamano hilo linalokwenda sambamba na kumbukumbu ya miaka 75 tangu kambi ya mauaji ya Auschwitz ilipokombolewa, Putin amesema wanawakumbuka wahanga wote wa mauaji hayo yaliyofanywa na utawala wa Kinazi wakiwemo Wayahudi milioni sita ambao walikufa katika makambi.

Israel Jerusalem | 75. Jahrestag Befreiung von Auschwitz | World Holocaust Forum | Wladimir Putin, Präsident Russland
Rais wa Urusi, Vladmir Putin akihutubia katika kongamano la JerusalemPicha: Getty Images/AFP/R. Zvulun

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema ghasia dhidi ya Wayahudi zinaongezeka na zinachochewa na chuki pamoja na kutovumiliana.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amewataka viongozi ulimwenguni kukabiliana na Iran, akiilinganisha na utawala wa Kinazi nchini Ujerumani. Netanyahu ambaye ameitaja Iran kuwa yenye chuki kubwa dhidi ya Wayahudi, amemshuruku Rais wa Marekani Donald Trump na makamu wake Mike Pence, kwa kuweza kupambana na Iran.

Viongozi wengine watakaohutubia katika kongamano hilo ni pamoja na Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinemeir. Steinemeir anakuwa rais wa kwanza wa Shirikisho la Ujerumani kuhutubia katika kumbukumbu za mauaji dhidi ya Wayahudi kwenye kituo cha Yad Vashem.

Rais wa Israel, Reuven Rivlin amewashukuru viongozi hao wa dunia kwa kuhudhuria kongamano hilo la Jerusalem na kuonyesha mshikamano na jamii ya Wayahudi.

Rais wa Poland Andrzej Duda ambako kambi ya Auschwitz ilijengwa wakati wa vita aliukataa mwaliko wa kuhudhuria kwa sababu Poland haikutakiwa kuhutubia katika kongamano hilo. Poland itafanya kumbukumbu yake katika eneo la makumbusho la Auschwitz-Birkenau Januari 27, kama ambavyo hufanya kila mwaka.

(AP, DPA, AFP, Reuters)