1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi duniani wampongeza Biden na Kamala

Grace Kabogo
21 Januari 2021

Viongozi mbalimbali duniani wameendelea kutoa salamu zao za pongezi kwa rais mpya wa Marekani, Joe Biden baada ya kuapishwa jana kuliongoza taifa hilo.

https://p.dw.com/p/3oE0x
USA Washington | Amtseinführung: Joe Biden und Kamala Harris
Picha: Kevin Dietsch/AP/picture alliance

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel amempongeza Biden na makamu wake, Kamala Harris ambao wanahitimisha utawala wa miaka minne uliokuwa na misukosuko chini ya Donald Trump. Michel amesema ni muda wa kurejesha uhusiano wa maana na wenye busara kati ya umoja huo na Marekani. Kwa upande wake Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema Ulaya iko tayari kuanza upya.

Suala la nyuklia

Rais wa Iran, Hassan Rouhani amepongeza kuondoka kwa Trump na amerudia kuitolea wito Marekani kuondoa vikwazo ilivyoweka kutokana na shughuli zake za nyuklia.

''Tunatarajia utawala wa Biden utatekeleza ahadi zake chini ya azimio namba 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kujaribu katika miaka minne ijayo. Kama watatekeleza ahadi yao, na sisi tutatekeleza ahadi yetu,'' alifafanua Rouhani.

Utawala wa Biden unataka kuirejesha Marekani katika makubaliano ya nyuklia ambayo Trump alijiondoa.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amemsihi Biden kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili. Naye Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg amesema ushirikiano kati ya muungano huo na Marekani ni msingi wa usalama wao, na NATO imara ni bora kwa Amerika Kaskazini na Ulaya.

Vatikan Petersdom Papst Franziskus Segen "Urbi et orbi"
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa FrancisPicha: Vatican Media/AP Photo/picture alliance

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amemtaka Biden kukuza upatanisho na amani ulimwenguni kote. Papa amesema anamuombea maamuzi yake yaongozwe na utashi wa kuijenga jamii inayojulikana kwa haki na uhuru. Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema anatazamia mwanzo mpya wa urafiki kati ya Ujerumani na Marekani pamoja na ushirikiano. Hayo ameyazungumza baada ya kumpongeza Biden pamoja na Harris, akisema ushindi wao ni demokrasia ya kweli ya Marekani.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amewatakia watu wa Marekani kila la heri katika siku muhimu. Macron amesema watafanya kazi pamoja kukabiliana na changamoto za wakati huu na kuilinda dunia. Naye Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson ambaye amekuwa akikosolewa kutokana na kuwa na uhusiano wa karibu na Trump, amesema anatazamia kufanya kazi kwa karibu na Biden.

Kushughulikia amani Mashariki ya Kati

Pongezi kama hizo zimetolewa pia na Urusi, Canada, India, Japan, Korea Kusini, Kuwait, Qatar, Bahrain, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Hata hivyo, kiongozi wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas amesema ana matumaini Marekani itakuwa na mwelekeo tofauti kuhusu mchakato wa amani na utulivu katika ukanda wa Mashariki ya Kati. Abbas alimkosoa Trump kwa kuwa na upendeleo kuelekea Israel, baada ya kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem.

USA Washington | Inauguration | Joe Biden im Oval Office
Rais mpya wa Marekani, Joe Biden akisaini maagizo kadhaaPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Wakati pongezi hizo zikimiminika, Biden ameanza kazi kwa kusaini maagizo kadhaa ya kiutendaji kuhusu masuala ambayo hayahitaji idhini ya bunge ikiwemo kuirejesha Marekani katika Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi. Marekani ilijiondoa rasmi katika mkataba huo, Novemba mwaka uliopita. Macron alimkaribisha tena Biden katika makubaliano hayo.

Maagizo mengine ya kiutendaji yaliyosainiwa na Biden siku yake ya kwanza madarakani, ni pamoja na kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona na uchumi wa Marekani unaodorora.

(AFP, AP)