1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia walaani shambulio la Uingereza

Iddi Ssessanga
23 Machi 2017

Viongozi wa dunia wameungana pamoja kulaani shambulio lililofanywa katikati mwa jiji la London Jumatano na mwanaume ambaye baadaye alipigwa risasi na kuuawa na polisi, ambapo wengi wameelezea mshikamano na Uingereza.

https://p.dw.com/p/2ZnFI
Großbritannien Theresa May Downing Street in London
Picha: Reuters/R. Pohle

Katika taarifa nje ya ofisi yake ilioko Mtaa wa Downing, waziri mkuu wa Uingereza Theresa May alilielezea shambulio hilo kuwa la kuchukiza na potovu, na kusema kuwa mshambuliaji huyo alichaguwa eneo la bunge kama mashambulizi dhidi ya  maadili ya kidemokrasia ya Uingereza.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema Ujerumani inasimama thabiti na imara pamoja na Waingereza katika mapambano dhidi ya aina zote za ugaidi, huku rais Frank-Walter Steinmeier akiongeza kuwa: "Katika nyakati hizi za hatari, sisi Wajerumani tuko karibu zaidi na watu wa Uingereza.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande alituma ujumbe wa mshikamano na kuunga mkono watu wa Uingereza, akisema Ufaransa inaelewa maumivu yao baada ya shambulio hilo, ambamo wanafunzi watatu wa Kifaransa walijeruhiwa pia.

Großbritannien Terroranschlag in London | Westminster Bridge am Tag danach
Maafisa wa polisi wakiwa kwenye daraja la Westminster asubuhi baada ya shambulio la lililofanywa na mwanaume aliekuwa akiendesha gari na kushika kisu, ambapo watu watano waliuawa.Picha: Reuters/D. Staples

Ikulu ya Marekani pia ililaani shambulio hilo na kuahidi msaada kamili wa serikali ya Marekani katika kujibu shambulio hilo na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria, alisema Sean Spicer, msemaji wa ikulu hiyo ya White House mjini Washington.

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau aliandika kwenye ukurasa wake wa twita kuwa: Hisia zetu ziko pamoja na waathirika wa shambulio la London pamoja na familia zao. Wacanada wanaendelea kuwa pamoja na watu wa Uingereza.

Juncker: Ni ugaidi

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, alisema shambulio limemkumbusha Brussels, ambako magaidi wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu waliuwa watu 32 katika mashambulizi mawili dhidi ya uwanja wa ndege na kito cha reli mwaka mmoja uliopita.

"Hili ni shambulio la kigaidi na halibadilishi chochote kwa walioathirika. Tuko pamoja na waathirika, na hii ni siku maalumu mjini Brussels, nchini Ubelgiji, kwa sababu mwaka mmoja uliopita, mwaka mmoja kamili uliopita, tulikuwa na mashambulio mjini Brussels," alisema Junckers mjini Brussels alikokuwa kuadhimisha mwaka mmoja tangu mashambulizi ya 2016.

Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk alisema kupita ukurasa wake wa twitter kuwa Ulaya inasimama pamoja na Uingereza dhidi ya ugaidi na iko tayari kusaidia. Urusi nayo kupitia msemaji wa wizara yake ya mambo ya nje ilituma ujumbe wa rambirambi. Waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte aliiambia televisheni ya Kidachi kwamba alistushwa na habari za kutisha na kusema wanaomboleza pamoja na London.

Großbritannien Bewaffnete Polizei nach Terroranschlag in London
Askari polisi wakilinda doria mbele ya jengo la bunge la Uingereza katikati mwa London Machi 22, kufuatia shambulio la kigaidi lililogharimu maisha ya watu watano na kujeruhi zaidi ya 40.Picha: picture-alliance/Kyodo

Waziri Mkuu wa Italia Paolo Gentilon, ambaye alinyamaza kwa muda mwanzoni mwa mkutano wa wabunge wa chama cha Social Democratic, alituma salamu za rambirambi pia. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisisitiza kuwa Uturuki inahisi na kushiriki kikamilifu katika maumivu ya Uingereza na inasimama pamoja na nchi hiyo katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Mawaziri wakuu wa uhispania Mariano Rajoy, wa Australia Malcom Turnbull, wa China Li Keqiang na wizara ya mambo ya nje ya Singapore wote waliezelea mshikamano na Uingereza, huku Qatar ikisisitiza msimamo wa kupinga vurugu za kila aina na kuelezea kuiunga mkono Uingereza katika hatua zake zote za kuhakikisha usalama katika wakati huu mgumu. Rais wa Venezuela Nicolas Maduro pia alisema anaungana na watu wa  London na kupinga aina zote za ugaidi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,ape.

Mhariri. Daniel Gakuba