1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G7 waahidi dozi bilioni 1 dhidi ya COVID-19

John Juma
13 Juni 2021

Viongozi wa G7 wamaliza mkutano wa kilele huku wakiahidi dozi bilioni moja ya chanjo dhidi ya COVID-19 kwa nchi masikini.

https://p.dw.com/p/3upKD
England | G7 Gipfel 2021
Picha: Phil Noble/REUTERS

Mkutano wa kilelele wa siku tatu wa mataifa yenye nguvu kubwa ya uchumi wa kiviwanda duniani G7 umemalizika nchini Uingereza. Viongozi wa nchi hizo wameahidi dozi bilioni moja ya chanjo dhidi ya virusi vya corona kwa mataifa masikini katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.

Aidha wametoa wito wa haraka kusitishwa mzozo wa jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.

Kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, viongozi hao wametambua suala hilo kuwa suala linalozidisha ukosefu wa usawa na kitisho kinachozidi kuongezeka ulimwenguni.

Wamekariri ahadi yao ya kuachana kabisa na matumizi ya nishati visukuku ifikapo mwaka 2025. Aidha wameahidi kulinda na kuhifadhi sehemu kadhaa za ardhini na baharini katika miongo ijayo.

Masuala mengine ambayo viongozi hao walijadili ni pamoja na wito wa kulinda haki za binadamu katika baadhi ya mataifa ikiwemo China, uchumi wa ulimwengu pamoja na wito wa kukommesha udukuzi unaodaiwa kufanywa na Urusi.

Angela Merkel: Joe Biden ameleta hamasa mpya katika G7

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) na Rais wa Marekani Joe Biden (kulia)
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) na Rais wa Marekani Joe Biden (kulia)

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema rais wa Marekani Joe Biden ameleta hamasa mpya katika juhudi za kukabili changamoto zinazoikumba dunia.

Amesema hayo Jumapili wakati wakuu wa nchi zilizostawi kiviwanda na tajiri zaidi ulimwenguni za kundi la G7 wakimaliza mkutano wao wa kilele mjini Cornwall kusini magharibi mwa Uingereza

"Si kwamba ulimwengu hauna tena matatizo kwa sababu ya kuchaguliwa kwa Joe Biden kuwa rais wa Marekani. Lakini tunaweza kutafuta suluhisho la matatizo hayo kutumia nguvu mpya, na ninafikiri ni vizuri kwamba tumekuwa imara zaidi tena kama G7,” Merkel aliwaambia waandishi wa habari.

Soma pia: Mataifa ya G7 kuanzisha mpango wa uwekezaji utakaoshindana na wa China

Mkutano huo wa kilele wa G7 ulikuwa wa kwanza kwa Rais Biden tangu alipochaguliwa rais na umetajwa kama nafasi ya kujenga upya mahusiano yaliyozorota baada ya miaka minne ya rais  wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Mkutano huo ulijikita zaidi kwenye janga la COVID-19 na mabadiliko ya tabia nchi.

Merkel asifia uamuzi wa kuirejehesha Marekani kwenye mkataba wa Paris

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Leon Neal/AP Photo/picture alliance

Merkel amesema uamuzi wa Biden kuirejesha Marekani katika mkataba wa Paris wa kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi ulifanya uamuzi kuwa rahisi wakati wa mazungumzo yao mkutanoni kuliko hapo awali.

Merkel ambaye pia alifanya mkutano wa ana kwa ana na Biden pembezoni mwa mkutano huo wa Cornwall amemkaribishwa na rais huyo wa Marekani ili azuru ikulu ya White House Julai 15.

Kwa Merkel, mkutano wa mwaka huu wa G7 ulikuwa wake wa 15 na wa mwisho kwake kuhudhuria kama kansela wa Ujerumani. Mwanasiasa huyo wa muda mrefu wa Ujerumani anapanga kustaafu baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Septemba.

Amesifia matokeo ya mkutano huo kuhusu suala la mabadiliko ya tabia nchi akisema yanadhihirisha uimara wa nchi kujitolea kukabili suala hilo japo nchi tajiri kiviwanda hazikuweza kuafikiana kuhusu tarehe ya kutokomeza kabisa matumizi ya mkaa wa mawe.

Ujerumani kuongeza msaada wake kwa nchi maskini

Msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema nchi yake itaongeza mchango wake wa ufadhili kwa nchi maskini kutoka euro bilioni 4 hadi kima cha euro bilioni 6 kila mwaka ifikapo mwaka 2025.

Viongozi wa G7 wakikutana Cornwall Uingereza Juni 11, 2021
Viongozi wa G7 wakikutana Cornwall Uingereza Juni 11, 2021Picha: Koji Ito/Yomiuri Shimbun/picture alliance

Amesema hayo baada ya kansela Merkel kusisitiza umuhimu wa kujitolea kukabili changamoto za kiulimwengu, janga la COVID-19 na misaada ya miundo mbinu.

Nchi wanachama katika kundi la G7 ni pamoja na: Marekani, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Italia, Japan na Italia.