1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa maandamano Sudan waitisha tena maandamano

Sekione Kitojo
1 Mei 2019

Waandamanaji nchini Sudan wametoa wito wa kufanyika maandamano makubwa, wakisisitiza kuwa jeshi halina nia thabiti ya kukabidhi  madaraka kwa raia karibu wiki tatu baada ya kuuondoa madarakani uongozi wa Omar al-Bashir.

https://p.dw.com/p/3Hkwo
Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan
Picha: picture-alliance/AA

Wito  huo  unakuja  wakati  hali  ya  wasi  wasi  ikiongezeka kuhusiana  na  muundo wa  baraza jipya  la  pamoja  kati  ya  raia  na jeshi  litakaloiongoza  nchi  ya Sudan, wakati waandamanaji wakiimarisha  vizuwizi nje ya  makao makuu  ya  jeshi  katika mji mkuu  Khartoum. Pande  hizo  mbili  zina  mambo  mengi yanayokinzana  kuhusiana  na  wawakilishi  katika  baraza  hilo  jipya ambalo linatarjiwa  kuchukua  nafasi  ya  baraza  la  kijeshi  ambalo lilichukua  madaraka  baada  ya  kuondolewa  madarakani  Omar al-Bashir Aprili 11  baada  ya  maandamano  makubwa  ya  umma kupinga  utawala  wake  wa  miongo  mitatu.

Sudan Protestein Khartum
Maandamano mjini Khartoum kuupinga utawala wa al-BashirPicha: Getty Images/AFP/O. Kose

Jeshi limekuwa  likitaka  baraza  lenye  wajumbe 10  ikiwa  ni pamoja  na  wawakilishi  saba  wa  jeshi  na  raia  watatu.

Kutokubaliana  kumesababisha  Muungano kwa  ajili  ya  Uhuru  na mabadiliko  kutangaza  "maandamano  ya  watu  milioni  moja  hapo Mei 2 , siku  ya  Alhamis kusisitiza  dai lao kuu, ambalo ni utawala wa  kiraia".

"Baraza la  kijeshi  halina  nia thabiti  juu  ya  kukabidhi  madaraka kwa utawala  wa  raia," amesema  Mohamed Naji al-Assam , kiongozi wa  chama  cha  wanataaluma  wa  Sudan SPA  kilichoongoza maandamano.

"Baraza  la  kijeshi  linasisitiza  kwamba  baraza  la  pamoja linapaswa  kuongozwa  na  wanajeshi likiwa  tu  na  wawakilishi  wa kiraia," Assam  amesema, na  kuongeza  kuwa  jeshi  limekuwa likitaka  "kupanua  madaraka  yake  kila  siku".

"Jumuiya  ya  kimataifa  inapaswa  kuunga  mkono  uchaguzi  wa watu wa  Sudan." Mohammed al-Asam alisisitiza:

Sudan Khartum Proteste am Militärhauptquartier
Maandamano mengine ya watu milioni moja yameishwa na viongozi wa waandamanaji kudai serikali ya kiraiaPicha: Getty Images/AFP/A. Shazly

"Tunahisi kutokana  na vitendo vyote vya baraza la  kijeshi  la  mpito hadi wakati huu kwamba  halina nia ya  dhati  kuhamisha madaraka kwa raia, licha ya  uthibitisho  wa  baraza hilo wakati lilipoingia madarakani, likithibitisha kwamba limeingia madarakani kutokana  na madai ya umma na kuthibitisha  kwamba litahamisha  mamlaka kwa raia haraka iwezekanavyo. Sasa tunaona muda umepita wakati madaraka ya  baraza la  kijeshi yanaongezeka na hii ni  hatari kwa mapinduzi ya  Sudan."

Akizungumza  katika  mkutano  huo  huo  na  waandishi  habari , Madani Abbas Madani , kiongozi  mwingine  wa  maandamano, amelishutumu baraza  la  kijeshi  kwa  kutumia "lugha ya kuongeza mivutano ambayo  haishawishi ushirikiano".

Taarifa  zao  zimekuja  baada  ya  jenerali  mwandamizi  wa  jeshi  la Sudan  kutangaza  chombo  hicho  kipya  kwamba  kitaongozwa  na kiongozi  wa  sasa  wa  kijeshi  jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan
Abdel Fattah al-Burhan mkuu wa baraza la kijeshi linaloongoza Sudan Picha: picture-alliance/AA

Waandamanaji  wameliita  baraza  la  kijeshi  linaloongozwa  na Burhan "kuwa  ni  nakala  ya  utawala  ulioangushwa".

Wanataka  wingi  wa  raia  katika  baraza  litakalokuwa  na  wajumbe 15 pamoja  na  wanajeshi  ambapo kutakuwa  na  wawakilishi  saba kutoka  jeshini.

Katika mfarakano  unaoongezeka , baraza la  kijeshi  limesema wanajeshi  sita wameuwawa  katika  makabiliano  na  waandamanaji nchi  nzima  siku  ya  Jumatatu.