1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya watafuta njia ya kupata mfumo wa kupunguza utaratibu wa kupata maamuzi.

Sekione Kitojo22 Juni 2007

Viongozi wa mataifa ya umoja wa Ulaya waendelea na majadiliano kuhusu muswada wa mkataba, utakaowawezesha kuharakisha utaratibu wa kupata maamuzi katika kundi hilo lenye wanachama 27.

https://p.dw.com/p/CB3P
Angela Merkel rais wa sasa wa umoja wa Ulaya, wadhifa unaozunguka katika mataifa wanachama, anaonekana mbele ya bendera ya umoja huo, kabla ya mkutano mjini Brussels.
Angela Merkel rais wa sasa wa umoja wa Ulaya, wadhifa unaozunguka katika mataifa wanachama, anaonekana mbele ya bendera ya umoja huo, kabla ya mkutano mjini Brussels.Picha: AP/LU/Toms Grīnbergs/DW

Viongozi wa mataifa wanachama wa umoja wa Ulaya wako mjini Brussels kwa mazungumzo juu ya kutayarisha muswada wa mkataba , wenye lengo la kupunguza mfumo wa utaratibu wa utoaji maamuzi kwa kundi hilo lenye mataifa wanachama 27.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewaambia waandishi wa habari kuwa haitawezekana kusema iwapo wataweza kufikia makubaliano kuhusu mkataba huo mpya. Hata kabla ya viongozi hao kuwasili , Poland na Uingereza zimeonya kuwa zitatumia kura zao za turufu kuzuwia makubaliano.

Poland inasema kuwa mfumo uliopendekezwa wa upigaji kura utazipendelea nchi kubwa.

Waziri mkuu Jaroslav Kaczynski ameiambia redio moja kuwa Poland inahaki ya kupata nguvu zaidi kwasababu ingekuwa na idadi kubwa ya wakaazi kama si kwa athari ilizozipata kutokana na vita vikuu vya pili vya dunia. Hata hivyo baada ya duru ya kwanza ya majadiliano hapo jana , kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye ni rais wa umoja huo kwa sasa hakuweza kutaja vipengee vya majadiliano ambavyo vimekuwa vikisababisha mvutano.

Amesema kuwa kikao cha jioni kimemalizika na amefurahishwa sana , na wingi wa wawakilishi waliohudhuria, lakini wanatambua kuwa katika kikao hicho cha siku nzima ni kitu cha kawaida kuwa hakuna matokeo ya kutangazwa hadi sasa. Ameongeza kuwa hii ni duru ya kwanza ya kubadilishana mawazo. Mapendekezo yote yaliyopo yamezingatiwa.

Mkataba huo una lengo la kuchukua nafasi ya katiba ya umoja wa Ulaya iliyoshindikana, baada ya wapiga kura nchini Ufaransa na Uholanzi kuikataa katika kura ya maoni miaka miwili iliyopita.