1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMalta

Viongozi wa EU wahimiza kuchukuliwa hatua za kuzuia uhamiaji

30 Septemba 2023

Viongozi wa nchi tisa za Mediterania na kusini mwa Ulaya wamehimiza kufanyika kwa juhudi zaidi za Umoja wa Ulaya kukabiliana na suala tete la uhamiaji kuanzia mizizi yake, na nchi wanazotumia wahamiaji kuingia Ulaya.

https://p.dw.com/p/4WzUi
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kushoto) Waziri Mkuu wa Malta Robert Abela, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni katika mkutano mjini Valletta, Malta.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kushoto) Waziri Mkuu wa Malta Robert Abela, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni katika mkutano mjini Valletta, Malta.Picha: FILIPPO ATTILI/CHIGI PALACE/ANSA/picture alliance

Waziri Mkuu wa Italia mwenye kuegemea siasa za mrengo mkali wa kulia Giorgia Meloni amesema nchi ziliko kwenye mstari wa mbele zinakabiliwa na idadi kubwa ya wahamiaji, japo bila ya suluhu ya "kimuundo" kutoka Umoja huo, basi kila nchí italemewa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametoa wito wa "mwitikio wa pamoja wa Umoja wa Ulaya" akihimiza mshikamano na Italia na nchi zote ambazo huwa za kwanza kupokea wahamiaji.

Soma pia:Wahamiaji 46 na miili kadhaa yapatikana Mediterrania 

Viongozi wa nchi zinazojulikana kama "Med 9" walikutana nchini Malta kujadili juu ya kadhia ya wahamiaji, siku moja baada ya mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kuafikiana juu ya hatua mpya za kushughulikia suala la wahamiaji.

Kwa jumla, watu wapatao 186,000 waliwasili kwa njia ya bahari kusini mwa Ulaya kuanzia Januari hadi Septemba 24, katika nchi za Italia, Ugiriki, Cyprus, Malta na Uhispania.

Zaidi ya watu 130,000, waliingia Italia - idadi hiyo ikiashiria ongezeko la asilimia 83 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.