1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa siasa Kenya waruhusiwa kuingia Bomas

Grace Kabogo
14 Agosti 2022

Viongozi wa vyama vya siasa wanashusha pumzi kwa muda baada ya kuruhusiwa kuingia kwenye uwanja wa Bomas. Hata hivyo wamezuiliwa kuingia ukumbini yanakofanyiwa uhakiki matokeo ya uchaguzi wa rais.

https://p.dw.com/p/4FWAH
Kenia Wahlen 2022
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Wakati huo huo, mgombea wa urais wa chama cha Agano David Waihiga Mwaure amekuwa wa kwanza kukiri kushindwa katika uchaguzi huo huku matokeo yakisubiriwa.

Baadhi ya viongozi wa Azimio la Umoja One Kenya walizuiliwa kuingia kwenye ukumbi wa Bomas kwa muda walipofika hapo mchana huu. Viongozi hao ni pamoja na seneta mteule Edwin Sifuna, mbunge mteule wa Makadara George Aladwa, gavana mteule wa Siaya James Orengo, wakala mkuu wa mgombea wa urais Ndiritu Muriithi.

Chebukati atakiwa kuwa muwazi

Wakala huyo wa Azimio la Umoja, alimtaka mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, IEBC Wafula Chebukati kuwa muwazi.

Viongozi hao waliruhusiwa kuingia kwenye eneo hilo baadaye ila wamezuiliwa kuingia kwenye ukumbi ambako shughuli ya kujumlisha na kuhakiki matokeo ya uchaguzi wa rais inaendelea. Itakumbukwa kuwa Jumamosi usiku kamishna Abdi Guliye alitangaza kuwa wanaoruhusiwa kwenye sehemu hiyo ni mawakala, wasaidizi wao, waangalizi, wasimamizi wa IEBC na waandishi wa habari pekee.

Kenia Wahlen 2022
David Waihiga Mwaure, mgombea wa urais kupitia chama cha AganoPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Kwa upande mwengine, David Waihiga Mwaure mgombea wa urais kupitia chama cha Agano ndiye mgombea wa kwanza wa urais kukutangaza kuwa ameshindwa katika kinyang'anyiro hicho na kumuunga mkono William Ruto wa UDA.

Kwa mtazamo wake IEBC inapaswa kuikamilisha shughuli ya kuhakiki na kujumlisha matokeo ya urais kwa uwazi na usawa. Mwaure alisisitiza kuwa malengo ya UDA yanashabihiana na mtazamo wake wa utendaji.

Ruto awataka Wakenya kuwa na subra

Yote hayo yakiendelea, mgombea wa urais wa UDA William Ruto anawarai Wakenya kuvuta subra na kuipa nafasi tume ya uchaguzi kukamilisha wajibu wake. Akiwa kwenye ibada mtaani Karen kwenye makazi yake rasmi aliwashukuru Wakenya kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kwamba juhudi zao hazitaambulia patupu. Mgombea huyo wa urais wa Kenya Kwanza alisindikizwa na mgombea mwenza, Rigathi Gachagua.

Kwa upande mwengine, wanaharakati wa kijamii wanawatolea wito wanasiasa na wafuasi wao kujizuwia ili kuepusha wasiwasi ambao unaweza kuzua vurugu nchini. Kwenye taarifa yao ya pamoja, watetezi hao wa haki wanatahadharisha kuwa baadhi wanaitumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa kuhusu uchaguzi.