1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakutana Brussels

27 Juni 2014

Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels kujaribu kuupatia ufumbuzi mvutano uliosababishwa na Uingereza kuhusu kuteuliwa Jean-Claude Juncker kuwa mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja huo.

https://p.dw.com/p/1CRLB
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani (kushoto) akijadiliana jambo na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani (kulia) akijadiliana jambo na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.Picha: picture-alliance/dpa

Ingawa kila kitu kinadhihirisha uamuzi wa kumteuwa Juncker kushika nafasi itakayoachwa na mwenyekiti wa sasa wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, utapitishwa katika mkutano huo wa kilele, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amepania kufanya kila awezalo kutetea msimamo wake kuhusu mustakbali wa Umoja wa Ulaya.

"Si haki kwamba viongozi waliochaguliwa wa serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya waachilie mbali haki yao ya kumteuwa kiongozi wa halmashauri kuu. Ni muongozo mbaya na anayechaguliwa pia hafai. Jean-Claude Juncker ni mshika bendera wa mradi wa kuuzidishia madaraka Umoja wa Ulaya na kuyapunguzia madaraka mataifa wanachama. Yeye si mtu anaefaa kuiongoza halmashauri hii." Anasema Cameron

Majadiliano moto moto yanategemewa

Waziri Mkuu huyo wa Uingereza ameonya majadiliano yatakuwa makali kuhusu kuteuliwa waziri mkuu huyo wa zamani wa Luxembourg. Hata hivyo, ukakamavu wa Cameron unalinganishwa na mbio za sakafuni, maana anaungwa mkono na Waziri Mkuu wa Hungary tu, Viktor Orban, katika madai yake dhidi ya Juncker.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron (kushoto), na Jean Claude Juncker anayetarajiwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron (kushoto), na Jean Claude Juncker anayetarajiwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.Picha: picture-alliance/dpa

Viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya, tangu wa mrego wa kihafidhina mpaka wa mrengo wa shoto, wanamuunga mkono Juncker. Walipofika katika ukumbi wa mkutano, hakuna yeyote aliyesema chochote kuhusu hilo - si Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na wala Rais Francois Hollande wa Ufaransa.

Wito wa mageuzi unapingwa na wahafidhina

Licha ya lawama na vitisho vinavyotolewa na Cameron, viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya wanahisi muhimu ni mkakati na sio kiongozi anayeusimamia. "Uingereza inauhitaji Umoja wa Ulaya, sawa na vile ambavyo Umoja wa Ulaya unaihitaji Uingereza," amesema Waziri Mkuu wa Denmark, Helle Thorning-Schmidt.

Viongozi wa vyama vya Social Democratic barani Ulaya wamuunga mkono Jean Claude Juncker kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.
Viongozi wa vyama vya Social Democratic barani Ulaya wamuunga mkono Jean Claude Juncker kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.Picha: Reuters

Naye Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Elio Di Ripo, licha ya kukiri kwamba msimamo wa Uingereza unaeleweka na unastahiki sifa, lakini ameonya kwamba taifa hilo haliwezi peke yake "kuwazuwia wenzao 26 ambao wanamtaka Juncker."

Viongozi wa Social Democratic wakiongozwa na Rais Hollande wameelezea uungaji mkono wao kwa Juncker tangu mwishoni mwa wiki iliyopita. Hata hivyo, wanataka badala yake watu waregeze kamba katika baadhi ya masuala kama vile bajeti ili kuunga mkono uwekezaji na ukuaji wa kiuchumi. Lakini madai hayo yanakataliwa na wahafidhina wakiongozwa na Kansela Merkel.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef