1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vyawakimbiza Wasomali nchini kwao

Kabogo Grace Patricia29 Julai 2009

Raia hao wa Somalia uhatarisha maisha yao kusafiri kimagendo kwenda hadi Yemen

https://p.dw.com/p/Izk9
Baadhi ya wakimbizi wa Somalia wakipatiwa chakula katika eneo moja huko Yemen, mwaka 2007.Picha: AP/UNHCR, Jon Bjoergvinsson

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), limesema kuwa maelfu ya Wasomali wanahatarisha maisha yao kwa kusafiri kimagendo kwenda Yemen, ikiwa ni njia ya kuingia katika eneo la Mashariki ya Kati.

Roy Redmond, msemaji wa shirika hilo la wakimbizi, amesema watu hao wanavuka katika Ghuba ya Aden kukimbia vita baina ya wapiganaji wa Kiislamu na majeshi ya serikali ya Somalia. Kiasi cha watu 12,000 wamejihifadhi katika makaazi ya muda huko Bossaso, kaskazini mwa Somalia na wanampango wa kuwalipa wanaofanya biashara ya magendo kwa ajili ya kusafirishwa na boti kwenda Yemen, wakati hali ya bahari inapokuwa nzuri katika mwezi Septemba. Hata hivyo, msemaji huyo wa UNHCR anasema kuwa wengi wa wanaosafiri kwa kutumia njia hiyo hufariki kama anavyoeleza Mwandishi habari wa Somalia, Hussein Aweis:

Kwa mujibu wa takwimu za shirika hilo la wakimbizi karibu Wasomali 300 ambao wangekuwa wahamaji, walikufa au hawajulikani walipo baada ya kulazimishwa kuruka majini mwaka 2008 na wengine zaidi ya 1,000 kuzama.

UNHCR na mashirika ya misaada yanajitahidi kuwashawishi wananchi wa Somalia kutopanda boti hizo za kimagendo ambazo ni hatari na pia kuwapatia chakula na dawa wale wanaobahatika kuwasili salama Yemen. Aidha, Yemen inawatambua Wasomali wote kama wakimbizi, lakini wengi wao wanaovuka Ghuba ya Aden huwa wanaingia katika nchi jirani za Saudi Arabia na Oman kwa lengo la kutafuta kazi.

Yemen, nchi yenye watu milioni 23, ni asili ya mababu wa kiongozi wa mtandao wa kigaidi Al-Qaeda, Osama bin Laden. Serikali ya nchi hiyo inafanya jitihada za kukabiliana na kundi la kiislamu linalofanya vitendo vya kuwateka raia wa nchi za Magharibi.

Wakati hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Hillary Clinton anapanga kukutana na Rais wa serikali ya mpito ya Somalia wakati wa ziara yake ya siku saba barani Afrika wiki ijayo. Bibi Clinton atakuwa ni afisa wa kwanza wa ngazi ya juu kukutana na Rais wa Somalia, Sheikh Sharif Ahmed, ikionyesha nia ya utawala wa Rais Baracka Obama wa kuiunga mkono serikali hiyo isiyotawaliwa na sheria katika Pembe ya Afrika. Akizungumzia ziara hiyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Marekani, Ian Kelly, amesema mazungumzo baina ya viongozi hao wawili yatafanyika kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Agosti 5. Baada ya kutembelea Kenya, Bibi Clinton ataelekea nchini Afrika Kusini, Angola, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Nigeria, Liberia na Cape Verde.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri: M. Abul-Rahman