1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vuta N'kuvute inaendelea baina ya Iran na Uengereza

2 Aprili 2007

Televisheni ya serekali ya Iran, al-Alam, inayotangaza kwa lugha ya Kiarabu, imeripoti leo kwamba mabaharia wote 15 wa Kiengereza waliokamatwa wamekiri kwamba wameingia katika bahari ya Iran kinyume na sheria.

https://p.dw.com/p/CHH4
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uengereza, Margret Beckett.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uengereza, Margret Beckett.Picha: AP

Dai hilo lilitolewa na kituo hicho cha televisheni ambacho matangazo yake yanaelekezwa kwa Ulimwengu wa Kirabu na sio Iran kwenyewe. Mkuu wa majeshi ya Iran alisema hapo Machi 24 kwamba mabaharia hao walikiri baada ya kuhojiwa kwamba waliingia katika bahari ya Iran kwa njia isiokuwa ya kisheria. Lakini hajasema kwamba wote 15 walikiri jambo hilo. Haijatajwa wapi kituo hicho cha televisheni cha al-Alam kimepata habari hiyo. Kituo hicho hadi karibuni kilionesha video mabaharia wanne kati ya hao 15 wakisema kwamba walikuwa katika bahari ya Iran wakati walipokamatwa. Jana kulioneshwa picha za wawili wa mabaharia hao, wakitumia ramani, wanaashiria mahala panapodaiwa walizingirwa na kukamatwa na mashua za kijeshi za Iran. Mmoja wa mabaharia hao alisema anaweza kufahamu kwa nini Iran imekasirika kwa wao kujiingiza katika bahari ya nchi hiyo. Mahabusu hao walisema walikuwa wanatendewa uzuri na Wa-Irani.

Serekali ya Uengereza imekanusha moja kwa moja kwamba wanajeshi wake hao waliingia katika bahari ya Iran, na ikasema mabaharia hao yaonesha walibinywa ili wakiri jambo hilo.

Shirika rasmi la habari la Iran liliripoti jumamosi iliopita kwamba balozi wa Iran mjini Mosko alisema mabaharia hao watashtakiwa kwa kwenda kinyume na sheria za kimataifa, lakini balozi huyo baadae aliyakana matamshi yake, akisema tu kwamba mkasa huo sasa umeingia katika hatua ya kisheria. Na sasa Shirika hilo la Iran linasema kutokana na mabadiliko yalioonekana mnamo siku mbili zilizopita katika siasa za makelele za serekali ya Uengereza, televisheni ya al-Alam sasa haitaonesha maelezo zaidi juu ya mahojiano waliofanyiwa mabaharia hao. Shirika hilo halijasema mabadiliko hayo ni yepi, lakini Uengereza ilisema jana kwamba inaendesha mawasiliano ya moja kwa moja na Iran.

Waziri wa ulinzi wa Uengereta, Des Browne, aliiambia televisheni ya Uengereza ya BBC kwamba Uengereza inafanya kila inachoweza kuutanzua mzozo huo kwa njia za kibalozi kwa upesi kama inavowezekana. Pia juzi waziri wa mambo ya kigeni wa Uengereza, Bibi Margret Beckett, alisema, na hapa ninamnukuu: kila mmoja anasikitika kwamba hali hii imetokea.

+Tungependa tuambiwe wapi watu wetu waliko. Na tunataka kuona matokeo.+

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, amesema Uengereza ingebidi iombe radhi. Maafisa wa Iran pia wameilaumu Uengereza kwa kulipeleka jambo hilo hadi katika vikao vya Umoja wa Mataifa. Jana wanafunzi wa Ki-Irani waliandamana mbele ya ubalozi wa Uengereza mjini Tehran uliokuwa unalindwa vikali na polisi wa kuzuwia fujo. Wanafunzi hao walitaka mabaharia wa Kiengereza waliokamatwa waadhibiwe.

Naye Rais George Bush wa Marekani, ambaye ameiunga mkono Uengereza katika majaribio yake ya kuona mabaharia hao wanaachwa huru, alisikika jana akisema:

+Mahabusu wa Kiengereza ni suala tete kwa sababu Wa-Irani wamewachukuwa watu hao ndani ya Bahari ya Iraq, na hiyo ni tabia isioweza kusameheka. Mimi nayaunga mkono kwa nguvu majaribio ya serekali ya Blair kulitanzua suala hilo kwa amani.

Marekani imelikataa shauri kwamba mabaharia hao 15 wa Kiengereza wanaweza wakabadilishwa na maafisa watano wa Ki-Irani wanaoshikiliwa bila ya kufanyiwa mashtaka na majeshi ya Marekani nchini Iraq tangu Januari mwaka huu.

Rais wa sasa wa Umoja wa Ulaya, Kansela Merkel wa Ujerumani, akiitembelea Israel hapo jana, alisema Ujerumani inaiunga mkono kamili Uengereza katika mzozo huu.