1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vya upinzani Uganda vyaitisha maandamano ya amani

24 Februari 2011

Wapinzani wanataka uchaguzi mpya ufanyike Uganda wakidai kutokea mizwengwe katika uchaguzi uliopita

https://p.dw.com/p/10P6H
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza BesigyePicha: dpa

Wagombea urais walioshindwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Ijumaa iliyopita nchini Uganda, leo wametoa wito kufanyike maandamano ya amani kupinga matokeo ya uchaguzi wanaosema ulikumbwa na wizi wa kura. Kiongozi wa muungano wa vyama vinne vya kisiasa, Warren Kizza Besigye Kifefe, aliyeshinda asilimia 26 ya kura, na kushindwa na mpinzani wake rais Yoweri Museveni aliyepata asilimia 68 ya kura, amewahutubia mamia kadhaa ya wafuasi wake mjini Kampala na kuitisha uchaguzi mpya ufanyike.

Besigye ameieleza tume ya uchaguzi kuwa isiyo na umakini katika kazi yake na kuongeza kuwa chaguzi chini ya utawala wa rais Museveni ziligubikwa na wizi wa kura. Msemaji wa jeshi la Uganda, Felix Kulaije ameupuuza mwito wa Besigye akisema jeshi liko tayari kukabiliana nao. Rais Museveni ameapa kumkamata yeyote atakayejaribu kufanya maandamano mfano wa yale yaliyofanyika nchini Misri.