1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waafghanistan wapiga kura kwa shauku

5 Aprili 2014

Wananchi wa Afghanistan wamejitokeza kwa wingi Jumamosi (05.04.2014) yakiwemo maeneo ya hatari kumchaguwa mtu wa kuchukuwa nafasi ya Rais Hamid Karzai katika makabidhiano ya kwanza ya madaraka kwa njia ya kidemkrasia.

https://p.dw.com/p/1Bccg
Rais Hamid Karzai akipiga kura yake mjini Kabul.(05.04.2014)
Rais Hamid Karzai akipiga kura yake mjini Kabul.(05.04.2014)Picha: Reuters

Wananchi wa Afghanistan wamejitokeza kwa wingi Jumamosi(05.04.2014) kumchaguwa mtu wa kuchukuwa nafasi ya Rais Hamid Karzai katika makabidhiano ya kwanza ya madaraka kwa njia ya kidemokrasia wakati vikosi vinavyoongozwa na Marekani vikikamilisha vita vyao vya miaka 13 nchini humo.

Licha ya vitisho vya kundi la Taliban upigaji kura kwa kiasi kikubwa ulifanyika kwa amani huku kukiwa na misururu mirefu katika miji nchini kote wakati wapiga kura wakipiga kura zao chini ya ulinzi mkali takriban katika vituo 6,000.

Taliban imeukataa uchaguzi huo kuwa ni njama ya kigeni na imewataka wapiganaji wake kushambuliwa wafanyakazi wa uchaguzi,wapiga kura na vikosi vya usalama lakini hakuna shambulio lolote kubwa lililorepotiwa wakati wa mchana.

Mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) Ahmad Yusuf Nuristani ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu wengi wamejitokeza kupiga kura kuliko vile ilivyotarajiwa lakini hakutaja idadi bali amesema idadi hiyo ni ndogo katika maeneo ya vijijini kulinganisha na mijini.

Ameongeza kusema kwamba wamepata taarifa ya kupungukiwa na makaratasi ya kupiga kura na ameviagiza vituo vya majimbo kutowa makatarasi zaidi ya kupigia kura.

Vituo vya kupigia kura vimeanza kufungwa baada ya saa tano za kupiga kura, hapo awali ilitangazwa kwamba watu walioko kwenye misururu ya kupia kura wataendelea kupiga kura zao.

Mjini Kabul ambapo kulikuwepo na mfululizo wa mashambulio wakati yaliosababisha maafa wakati wa kampeni za uchaguzi,mamia ya watu wamepiga misururu hadharani kupiga kura licha ya kuwepo kwa mvua kubwa na ahadi ya waasi kuvuruga uchaguzi huo kwa matumizi ya nguvu.

Akina mama wakiwa katika msururu wa kupiga kura mjini Kabul. (05.04.2014)
Akina mama wakiwa katika msururu wa kupiga kura mjini Kabul. (05.04.2014)Picha: picture alliance/ZUMA Press

Laila Neyazi mama wa nyumbani mwenye umri wa miaka 48 amekaririwa akisema "Siogopi vitisho vya Taliban kwani kwa vyo vyote vile iko siku tutakufa. Nataka kura yangu iwe muadhara kwa Taliban."

Usalama katika uchaguzi huo lilikuwa suala lililozusha wasi wasi mkubwa kufuatia mashambulizi mjini Kabul likiwemo la Jumatano lililouwa askari polisi sita.

Mashambulizi yasababisha maafa

Mkuu wa IEC Nuristani amesema mashambulizi au hofu ya kuzuka matumizi ya nguvu vimelazimisha kutofunguliwa kwa vituo 211 kati ya 6,423.

Siku moja kabla ya uchaguzi huu mpiga picha wa shirika la habari la AP Anja Niedringhaus aliuwawa kwa kupigwa risasi na kamanda mmoja wa polisi katika jimbo la mashariki la Khost.

Huyo ni mwandishi wa tatu anayefanyakazi na vyombo vya habari vya kimataifa kuuwawa wakati wa kampeni za uchaguzi baada ya kuuwawa kwa mwandishi habari wa Sweden Nils Horner na Sardar Ahmad wa shirila la habari la AFP.

Waziri wa mambo ya ndani Omar Daudzai amesema kikosi kizima cha Afghanistan cha askari 400,000 wa polisi,jeshi na wanausalama wamewekwa kuhakikisha usalama nchini kote.

Msururu wa wapiga kura huko Mazar.(05.04.2014).
Msururu wa wapiga kura huko Mazar.(05.04.2014).Picha: DW/N.Asir

Waafghanistan wamechukuwa majukumu ya usalama mwaka huu kutoka vikosi vinavyoongozwa na Marekani mwaka ambao ni wa mwisho kwa vikosi vya muungano vya Jumuiya ya Kujihami ya NATO vya wanajeshi 51, 000 wa mapambano kuondoka nchini humo na kuwaachilia vikosi vya nchi hiyo kupambana na uasi wa kundi la Taliban bila ya msaada wao.

Katika mji wa magharibi wa Herat misururu ya mamia ya watu ilikuwa ikisubiri kupiga kura katika kituo kimoja cha kupigia kura wakati huko Jalalabad mashariki mwa nchi hiyo wapigaji kura walikuwa wakisubiri kwa uvumilivu nje ya msikiti mmoja.

Wapiga kura pia walikuwa katika misururu katika mji wa Kandahar ngome ya Taliban kusini mwa nchi hiyo baadhi ya wanawake wakiwa miongoni mwa wapiga kura kinyume na ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2009 ambapo idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilikuwa ndogo sana kutokana na hali mbaya ya usalama.

Uchaguzi huu wa rais wa tatu nchini humo unakamilisha miaka 13 ya utawala wa Karzai ambaye amekuwa madarakani tokea Taliban walipopinduliwa hapo mwaka 2001.

Wagombea wakuu

Takriban watu milioni 13.5 wana haki ya kupiga kura kutoka idadi ya watu wa nchi hiyo inayokadiriwa kufikia milioni 28.

Mkongwe akitumia haki yake ya kupiga kura Kabul.(05.04.2014).
Mkongwe akitumia haki yake ya kupiga kura Kabul.(05.04.2014).Picha: DW/Q.Wafa

Ziada ya duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi wa rais,wapiga kura pia wanayachaguwa mabaraza ya majimbo.

Wagombea walioko mstari wa mbele kuwania nafasi inayoachwa na Karzai ni waziri mkuu wa zamani wa mambo ya nchi za nje Zalmai Rassoul na Abdullah Abdullah ambaye alikuwa mshindi wa pili katika uchaguzi mwa mwaka 2009 na mwanataaluma wa Benki ya Dunia Ashraf Ghani.

Hakuna anayewekewa matumaini makubwa ya kushinda na iwapo hakuna mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika duru hiyo ya kwanza ambapo matokeo ya awali yanatarajiwa kutangazwa hapo tarehe 24 mwezi wa Aprili,marudio yatafanyika mwishoni mwa mwezi wa Mei.

Udanganyifu mkubwa na matumizi ya nguvu yaliozagaa yalitia dosari kuchaguliwa tena kwa Karzai hapo mwaka 2009 na matokeo yatakayobishiwa safari hii yatazidi kuzidisha changamoto zinazomkabili rais mpya.

Yoyote atakayeibuka mshindi itabidi aongoze mapambano dhidi ya Taliban bila ya msaada zaidi wa vikosi vya Jumuiya ya Kujihami ya NATO na pia kuimarisha kujitegemea kiuchumi kutokana na kupunguwa kwa misaada ya fedha.

Uchaguzi huyo yumkini ukatowa fursa kwa Afghanistan kuboresha uhusiano wake na Marekani ambayo ni mfadhili wake mkuu baada ya miaka mingi ya kigeugeu cha Karzai.

Uhusiano huo ulizidi kudhoofika mwishoni mwa mwaka jana wakati Karzai alipogoma kusaini makubaliano ya usalama ambayo yangeliiruhusu Marekani kubakisha kama wanajeshi 10,000 nchini Afghanistan kuwapatia mafunzo wanajeshi wa nchi hiyo na kuliandama kundi la Al Qaeda.

Mwandishi :Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri:Sekione Kitojo