1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji wawili wauawa nchini Bahrain

17 Februari 2011

Watu wawili wameuliwa na polisi mjini Manama nchini Bahrain kufuatia maandamano yanayoendelea tangu jumatatu katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba

https://p.dw.com/p/10ICv
Waaandamanaji katika uwanja wa Lulu mjini ManamaPicha: AP

Waandamanaji wawili wameuawa mapema leo katika mji mkuu wa Bahrain, Manama baada ya polisi kuchukua hatua za kuwaondoa waandamanaji waliokusanyika kati kati ya mji mkuu ,Manama.

Watu hao wametambulika kuwa ni Mahmoud Makii aliekuwa na umri wa miaka 22 na Ali Mansour Ahmad Khoder aliekuwa na umri wa miaka 52. Lakini jamaa zao hawakutoa habari zaidi juu namna walivyouawa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari watu wengine wasiopungua 50 walijeruhiwa.Na kati ya hao, 10 wamo katika hali mbaya.

Bahrain Proteste Opposition Sheik Ali Salman
Kiongozi wa chama cha upinzani cha washia Ali SalmanPicha: AP

Ndugu wa watu hao wawili waliouawa ni pamoja na wanawake waliokuwa wanalia mbele ya mlango wa kuingilia katika hospitali ya Salmaniya-hospitali kuu ya mji wa Manama.

Mashirika ya habari yamearifu kwamba majeshi ya usalama ya Bahrain yaliwashambulia waandamanaji waliokusanyika katika sehemu ya kati ya mji mkuu wa Bahrain, Manama ambapo walipiga kambi ya mahema kwenye uwanja wa Manama.

Walioshuhudia kadhia hiyo waliliambia shirika la habari la AFP kwamba maafisa wa usalama waliwashambulia waandamanaji kwa mabomu ya machozi ili kuwatimua kutoka kwenye uwanja wa Manama ambapo walikusanyika.Watu hao walikimbia kutoka kwenye uwanja huo huku wakikimbizwa na maafisa wa usalama Polisi pia walitumia helikopta.

Maalfu ya watu wamekuwa wanafanya maandamano kwenye uwanja wa Manamo tokea jumanne iliyopita baada ya polisi kuwaua waandamanaji wawili wa kishia walioshiriki katika harakati za kuipinga serikali.

Watu wa jamii ya washia ambao ni wengi nchini Bahrain wanahisi kubaguliwa na wasuni wa tabaka la juu.

Mwandishi:Abdul Mtullya

Mpitiaji:Hamidou Oummilkheir