1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waangalizi waukosoa mwenendo wa uchaguzi wa Uturuki

Josephat Charo
25 Juni 2018

Waangalizi wa kimataifa wamesema leo kwamba vyombo vya habari na utawala wa hali ya hatari vilichangia kubadili mkondo wa matokeo ya uchaguzi kumpendelea rais Recep Tayyip Erdogan.

https://p.dw.com/p/30FLn
Türkei |  Pressekonferenz der OSCE zur Türkeiwahlen
Picha: picture-alliance/dpa/NurPhoto/D. Cupolo

Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi uliofanywa na waangilizi wa shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya, OSCE na kitengo cha bunge cha baraza la Ulaya, PACE, rais Erdogan na chama chake cha AKP walinufaika kutokana na mazingira ya kisheria yaliyopo Uturuki. Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa shirika la OSCE, Ignacio Sanchez Amor, amesema haki za vyombo vya habari, uhuru wa kutoa maoni na kufanya mikutano ulibanwa chini ya utawala wa hali ya hatari.

"Katika uchaguzi huu, wapiga kura walikuwa na chaguo muhimu licha ya kukosekana mazingira ya ushindani katika wizani sawa. Rais aliye madarakani na chama chake walinufaika kutokana na nafasi yao na hili lilionekana kupitia taarifa nyingi za vyombo vya habari vya serikali na kibinafsi. Mfumo wa sheria na madaraka chini ya utawala wa hali ya hatari uliubarana uhuru msingi wa kukusanyika na kutoa maoni, hata uhuru wa vyombo vya habari."

Uchaguzi haukuwa wa haki

Igancio aidha amesema uchaguzi wa Uturuki haukuwa wa haki, akisema zaidi ya vyombo 300 vya habari vilionekana kuegemea upande wa serikali na kwamba viliripoti sana kuhusu mikutano ya Erdogan na chama chake cha AKP.

Igancio pia amedokeza kwamba wabunge wawili wenye uzoefu wa miaka mingi waliokuwa sehemu ya ujumbe wa shirika la OSCE waliarifiwa watanyimwa visa ya kuingia Ututruki walipokuwa wakisafiri kwa njia ya ndege kuelekea Ankara. Hatimaye walilazimika kurejea nyumbani.

Türkei - Wahlen
Wanawake wakisubiri kupiga kura wakati wa uchaguzi mjini Istanbul (24.06.2018)Picha: Reuters/H. Aldemir

Hata hivyo katika hatua ya kutia moyo, muangilizi kutoka kitengo cha bunge cha baraza la Ulaya, PACE, Olena Sotnyk, amesema licha ya mapungufu yaliyoshuhudiwa katika uchaguzi wa Uturuki, watu wengi walijitokeza kupiga kura zao.

"Bila shaka uchaguzi wa jana ulikuwa na umuhimu mkubwa. Kwanza ulieleweka kwa sababu ya idadi kubwa ya wananchi walioshiriki. Na hili lilidhihirishwa na idadi kubwa ya wapiga kura waliojitokeza. Nadhani hii ndilo jambo zuri chanya tunalohitaji kulitaja."

Hata hivyo waangalizi wamekosoa uwepo wa polisi katika vituo vya kupigia kura kwamba ulitatiza shughuli kuliko ilivyokuwa katika chaguzi za nyuma. Olena amesema katika baadhi ya visa, polisi walichangia kujenga mazingira ya hofu na kukosekana usalama, na pengine shinikizo dhidi ya wapigaji kura na hata waangalizi wa kimataifa.

Mwandishi: Josephat Charo/afpe/dpae

Mhariri: Iddi Sessanga