1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waarabu waidhinisha pendekezo la Palestina UN

30 Desemba 2014

Mabalozi wa mataifa ya Kiarabu wameidhinisha pendekezo la Palestina kuhusu marekebisho ya azimio la Umoja wa Mataifa la kutaka Israel kuacha kuikalia kwa mabavu Palestina katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

https://p.dw.com/p/1ECFh
Wananchi wa Palestina wakiwa wameshika bendera za nchi hiyo
Wananchi wa Palestina wakiwa wameshika bendera za nchi hiyoPicha: SAID KHATIB/AFP/Getty Images

Balozi wa Jordan kwenye Umoja wa Mataifa, Dina Kawar, na mwakilishi wa mataifa ya Kiarabu kwenye Baraza la Usalama la umoja huo, amesema pendekezo hilo ambalo linapingwa vikali na Israel na Marekani, limeidhinishwa na wajumbe 22 wa mataifa ya Kiarabu.

''Kundi la mataifa ya Kiarabu linaliunga mkono pendekezo hilo na sasa wanayo nakala mpya ya marekebisho na wameridhishwa nayo na tutaliwasilisha leo kwenye sekretarieti,'' alisema Balozi Kawar. Aidha, aliongeza kuwa kuna suala la Jerusalem na masuala mengine yanayowahusu wafungwa, maji, makaazi na ukuta usio halali ambao ulikosolewa na mahakama ya kimataifa.

Balozi Kawar amesema viongozi wa Jordan na Palestina watakutana mapema iwezekanavyo kujadiliana kuhusu muda muafaka wa baraza la usalama kupiga kura, baada ya kuwasilisha rasimu ya mwisho ya azimio hilo.

Iwapo pendekezo hilo litapitishwa, Israel italazimika kuondoka kutoka kwenye maeneo inayoyakalia ya Palestina ifikapo Disemba 31 mwaka 2017.

Balozi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour
Balozi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyad MansourPicha: picture alliance/AP Photo

Hata hivyo, Marekani ambayo ni mshirika wa karibu wa Israel, inalipinga azimio hilo ikisisitiza kwamba lazima pawe na suluhisho la mazungumzo katika mzozo wa Israel na Palestina. Kura tisa za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinahitajika ili kulipitisha azimio hilo, lakini Marekani inaweza ikatumia nguvu yake kupiga kura ya turufu kulipinga.

Kura kupigwa karibuni

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Balozi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour amesema kura hiyo inaweza ikapagiwa leo (30.12.2014) au kesho (31.12.2014). Ingawa Balozi Kawar alipoulizwa kuhusu kura hiyo kusogezwa hadi Januari Mosi, amesema yote yanawezekana.

Wanadiplomasia kadhaa kutoka mataifa ya Magharibi wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wameshangazwa na uamuzi huo wa ghafla wa kuwasilisha muswada wa azimio hilo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Jeff Rathke amewaambia waandishi wa habari kwamba azimio hilo jipya siyo jambo ambalo wanaweza wakaliunga mkono na kwamba nchi nyingine zina mtazamo sawa na Marekani.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: AFP/Getty Images/G. Tibbon

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema iwapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haitolikataa azimio hilo, wao watalipinga. Amesema mamlaka ya Palestina inajaribu kuweka amri kwa Israel ambayo itadhoofisha usalama wa Israel na kuuweka mustakabali wake wa baadaye katika hatari. Amesema Israel itayapinga mazingira yatakayohatarisha maisha yake ya baadaye.

Pendekezo la awali la Palestina lilikuwa linataka Jerusalam uwe mji mkuu wa pamoja kati ya Israel na Palestina, lakini muswada wa mwisho unaeleza kuwa Jerusalem Mashariki utakuwa mji mkuu wa Palestina na unaitaka Israel kuacha ujenzi wa makaazi na kuwaachia wafungwa wa Kipalestina.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,RTRE,AFPE
Mhariri: Elizabeth Shoo