1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaArgentina

Waargentina wagoma, waandamana kumpinga Rais Milei

Bruce Amani
25 Januari 2024

Maelfu ya Waargentina wamefanya maandamano na wengine wengine kufanya mgomo katika hatua kubwa ya kuzipinga sera za kupunguza bajeti za Rais Javier Milei wiki chache tu baada ya kuingia madarakani.

https://p.dw.com/p/4beXO
Maandamano Argentina
Maandamano ya kupinga sera za kubana matumizi za Rais Javier Milei nchini Argentina.Picha: Marcelo Endelli/Getty Images

Umati mkubwa ulikusanyika Jumatano (Januari 24) nje ya bunge katikati ya mji mkuu, Buenos Aires, ikiwa ni mojawapo ya maandamano makubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika miaka ya karibuni.

Waandamanaji hao walikuwa wakiitikia wito wa mgomo ulioitishwa na chama kikuu cha wafanyakazi katika nchi hiyo ya Amerika Kusini, CGT.

Siku kumi baada ya kuingia madarakani mwezi Desemba, rais huyo mpya alitangaza msururu wa mageuzi mapana ambayo yalipunguza ulinzi wa wafanyakazi, yakaondoa ukomo wa udhibiti wa bei za bidhaa muhimu za matumizi, miongoni mwa mambo mengine.

Polisi ilisema karibu watu 80,000 walishiriki maandamano hayo, huku waandalizi wakisema idadi hiyo ilifika nusu milioni.