1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi Msumbiji warefusha makubaliano ya usitishaji vita

Sylvia Mwehozi
3 Januari 2017

Waasi nchini Msumbiji wametangaza kurefusha kwa miezi miwili makubaliano ya kusitisha vita baina yao na serikali na kuongeza matumaini ya kupatikana kwa amani baada ya machafuko ya mwaka jana kugharimu maisha ya watu.

https://p.dw.com/p/2VCg1
Afonso Dhlakama und Filipe Nyusi Mosambik
Picha: AFP/Getty Images/S. Costa

 

Rais wa taifa hilo Felipe Nyusi amesema makubaliano hayo ya Alfonso Dhlakama kiongozi wa Renamo ambacho ni kikundi cha wanamgambo na wakati huo chama cha upinzani kilichochaguliwa, yanaonyesha kwamba pande zote mbili zimeanza kuaminiana.

Mapigano mabaya baina ya serikali ya Frelimo na Renamo yalitishia kuzuka upya vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Msumbiji iliyomalizika miaka 20 iliyopita. Lakini Dhlakama amewaambia waandishi wa habari kuwa na namnukuu: "kumekuwa na baadhi ya matukio madogo lakini makubaliano ya siku saba ya kusitisha vita yamekwenda vyema, kwa hivyo natangaza kurefusha makubaliano ahyo kwa siku yningine 60 hadi Machi 4", mwisho wa kunukuu.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo makubaliano hayo yanalenga kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo mjini Maputo katika hali ya amani na utulivu kwa pande zote mbili.

Dhlakama anayeishi mafichoni katika milima ya Gorongosa katikati mwa Msumbiji, amesema vikosi vya Renamo havitaishambulia serikali wala upinzani.

RENAMO-Führer Afonso Dhlakama
Kiongozi wa RENAMO nchini Msumbiji Afonso Dhlakama Picha: António Cascais

Mwaka jana kasi ya vurugu iliongezeka na watu zaidi ya 15,000 walilazimika kukimbilia katika makambi ya serikali ama kwa ndugu zao na wengine kuvuka mpaka na kuingia Malawi ama Zimbabwe.

Tangazo hilo la makubaliano ya kusitisha mapigano lilikuja baada ya hatua kadhaa juu ya mchakato wa amani kusitishwa kwa muda usijojulikana kutokana na baadhi ya vikwazo ikiwemo kuuliwa kwa mpatanishi wa Renamo.

Rais Filipe Nyusi alisema Jumatatu (02.01.2017) kwamba makubaliano hayo yalikuwa "yenye matunda" kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha binafsi cha STV na akanukuliwa akisema uaminifu unajengwa na kwamba majeshi ya serikali hayajafanya mashambulizi dhidi ya Renamo.

Mwanadiplomasia mmoja aliyezungumza na shirika la habari la AFP amesema Dhlakama alikuwa tayari amedhoofika na hivyo kulazimika kufikia makubaliano ya kujaribu fursa ya mazungumzo ya amani, ambayo huenda yakafanyika chini ya upatanishi wa kimataifa unaoratibiwa na Umoja wa Ulaya.

Mosambik Maputo Präsident Filipe Nyusi
Raia wa Msumbiji Felipe Nyusi mara baada ya kuapishwa 2015Picha: picture-alliance/dpa/A. Silva

Kiongozi huyo wa waasi ametangaza makubaliano hayo baada ya mfululizo wa mazungumzo ya kwenye simu na rais Nyusi. Mapigano yamekuwa mara kwa mara yakitokea katika barabara kuu nchini humo kwa wapiganaji wa Renamo kushambulia misafara ya serikali na magari ya raia na wanajeshi nao wanatuhumiwa kufanya ukatili kwa kuwalenga waasi katika vijiji vya jirani.

Watu wengi waliokosa makazi wanasema wanajeshi wa serikali mara nyingi pia huwachukulia wanakijiji katika jimbo la kati kuwa wanawaunga mkono waasi.

Msumbiji bado inajaribu kuponya majeraha ya umwagaji damu wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya mwaka 1976-1992 ambapo watu zaidi ya milioni moja waliuawa baina ya Frelimo na Renamo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga