1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi Syria kuheshimu usitishwaji vita

Admin.WagnerD26 Februari 2016

Wakati zimebakia saa chache kabla ya hatua ya kusimamaiha mapigano kuanza kutekelezwa nchini Syria ndege za Urusi zimeendelea kufanya mashambulio.

https://p.dw.com/p/1I34H
Rais wa Syria Bashar al-Assad
Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: picture alliance/AP Photo/V. Salemi

Makundi karibu mia moja ya waasi yanayopambana na utawala wa Bashar al-Assad yamesema yatayatekeleza makubaliano ya kusimamisha vita kwa muda Makundi hayo yamesema yataheshimu makubaliano ya kusimamisha vita kwa muda, yaliyofikiwa baina ya Urusi na Marekani ingawa habari zinasema kuwa ndege za Urusi ziliendelea kufanya mashambulio nchini Syria.

Kamati kuu ya jeshi la waasi, HNC imesema wapiganaji wake wataacha kupigana kwa muda wa wiki mbili. Katika tamko lake kamati hiyo imeionya serikali ya Syria na washirika wake kutojaribu kuyatumia makubaliano yaliyofikiwa ili kuendelea na vitendo vya kiadui kwa kisingizio cha kupambana na magaidi. Serikali ya Syria pia imesema kuwa itaheshimu mapatano yaliyofikiwa.

Rais Obama amesema macho ya dunia nzima yataelekezwa Syria.Obama amesema hakuna mtu anaejidanganya kutokana na utata wa nchini Syria. Lakini Obama ameeleza kuwa ikiwa makubaliano yatatekelezwa umwagikaji damu utapungua na kuwezesha kufanyika mazungumzo juu ya kuleta suluhisho la kisiasa ili kumaliza vita nchini Syria na hivyo kuelekeza nguvu zote dhidi ya magaidi wa "dola la kiislamu"

Rais Obama amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya magaidi wa "dola la kiislamu" yataendelea.

Syrien Ruinen Homs
Picha: picture-alliance/dpa

Kwa upande wake Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema mchakato wa amani nchini Syria utakuwa mgumu lakini ameeleza kwamba hakuna njia nyingine za kuumaliza mgogoro huo. Rais Putin pia amesisitiza kuwa mashambulio dhidi ya makundi ya kigaidi yataendelea.

Kiongozi huyo wa Urusi ameeleza kwenye mkutano na maafisa waandamizi wa serikali kuwa mashambulio ya ndege yanayofanywa na ndege za Urusi tangu mwezi wa Septemba yanaekelezwa dhidi ya makundi ya magaidi tu. Hata hivyo wanaoikosa Urusi wanadai kwamba ndege zake zinawashambulia pia waasi wanaopambana na utawala wa Assad.

Urusi na Marekani zimekubaliana juu ya kusimamisha mapigano nchini Syria lakini mapatano hayo hayatayahusu makundi ya kigaidi.

Mwandishi:Mtullya Abdu

Mhariri Josephat Charo