1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Laurent Nkunda wako tayari kurejea nyuma

Oumilkher Hamidou18 Novemba 2008

Katika wakati ambapo juhudi za amani zimeshika kasi,majeshi ya serikali yapigana na wanamgambo wa Mai Mai mashariki ya Kongo Kinshasa

https://p.dw.com/p/FxSv
Wakimbizi katika kambi ya KibatiPicha: picture-alliance/ dpa


Mapigano yamepamba moto kati ya jeshi la jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na wanamgambo wa Mai Mai katika eneo muhimu la Kanyabayonga.Mapigano hayo yanatokea katika wakati ambapo  waasi wa Laurent Nkunda wanasema watakua tayari kurejea nyuma kilomita 40 toka nyanja mbili za mapigano ,mashariki mwa nchi hiyo,ili kufungua njia ya kupatikana amani.



Taarifa ya waasi wa CNDP imetolewa siku mbili baada ya mazungumzo kati ya Laurent Nkunda na mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,rais wa zamani wa Nigeria,Olusegun Obasanjo.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo,kamati ya kisiasa ya CNDP imekutana Jomba hii leo  na kuamua kuwarejesha nyuma wapiganaji wao hadi kilomita 40,toka uwanja wa mapigano wa Kanyabayonga-Nyanzale na pia uwanja wa Kabasha-Kiwanja.


Zaidi ya hayo waasi wa CNDP wanaitaka tume ya Umoja wa mataifa katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo-MONUC idhamini usalama wa maeneo hayo na kuhakikisha wanajeshi wa serikali hawaingii katika maeneo hayo.


 Lengo la uamuzi huo,wanasema waasi wanaoongozwa na Laurent Nkunda ni kufungua njia ya kupatikana amani na kurahisisha juhudi za upatanishi za mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa Olusegun Obasanjo.


Katika wakati ambapo waasi wameamua kurejea nyuma,mapigano makali yameripuka katika mji muhimu wa Kanyabayonga,katika eneo hilo hilo la mashariki,kati ya vikosi vya serikali na waasi wa Mai Mai wanaoelemea upande wa serikali.


Wakaazi wote wa mji huo wameyapa kisogo maskani yao na kukimbilia katika maeneo ya msituni.Ripota wa shirika la habari la Ufaransa AFP anasema mji huo wa wakaazi 50 elfu umejiinamia, nyumba kaadhaa zimevunjwa na maduka na ofisi za serikali zimefungwa.


Akihojiwa na shirika la habari la Ufaransa AFP,mkuu wa wanamgambo wa Mai Mai, jenerali Lafontaine amethibitisha mapigano hayo na kusema yametokea kwa "makosa ".


Wakati huo huo maradhi ya kipindu pindu yameenea katika eneo hilo la mapigano mashariki ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.


Shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia watoto UNICEF limesema katika taarifa yake iliyochapishwa mjini Geneva Uswisi hii leo,watu 127 zaidi wameambukizwa na maradhi hayo katika kijiji chja Ishaha,kaskazini mwa Goma.


Msemaji wa shirika la UNICEF Veronique Taveau amesema kesi hizo mpya za Cholera zinatia wasi wasi hasa kutokana na hali mbaya wanayokumbana nayo watu waliyoyapa kisogo maskani yao kutokana na mapigano.


Wiki iliyopita  shirika la afya la umoja wa mataifa WHO lilizungumzia juu ya  kesi zaidi ya elfu moja za watu walioambukizwa maradhi ya kipindu pindu mashariki ya Kongo Kinshasa.