1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa LRA kushtakiwa katika mahakama za Uganda

Kalyango Siraj13 Machi 2008

Rais Museveni asema wapiganaji wa LRA wanaweza kushtakiwa chini ya sheria za Uganda

https://p.dw.com/p/DNTh
Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Malkia Elizabeth II wa Uingereza walipokuwa Ikulu ya EntebbePicha: AP

Kiongozi wa Uganda,Yoweri Museveni, amesema kuwa wapiganaji wa kundi la uasi dhidi ya utawala wake la The Lord Resistance Army, LRA, ambao wanakabiliwa na kesi ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai,wanaweza badala yake wakafikishwa mbele ya mahakama za Uganda.

Kundi hilo limeendesha vita vya msituni dhidi ya utawala wa Museveni kwa miongo miwili na watu wengi wameuawa,wengine kupoteza viungo na wengi kupoteza makazi yao.

Na wajumbe wa serikali na wa waasi wamekuwa wanakutana mjini Juba ,Sudan Kusini, kujaribu kutanzua mgogoro huo,lakini kizuizi cha kupatikana kwa mkataba wa amani ni kesi hiyo ilioko katika mahakama ya kimataifa.

Rais Museveni,akiwa katika zaira ya kikazi nchini Uingereza,amewaambia wandhishi habari kuwa serikali yake imekubali kuwa wapiganaji wa kundi la LRA watashughulikiwa na sheria za nyumbani na wala sio za kigeni.Aidha amekanusha kuwa suala hilo ndilo kiungo muhimu cha kukomesha vita ambavyo vimedumu miaka 20 katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Kiongozi wa LRA, Joseph Kony, pamoja na maafisa wake wa ngazi za juu wanne wanatakiwa na mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ya mjini The Hague,Uholanzi,kwa makosa yanayohusina na uhalifu wa kivita. Miongoni mwa makosa hayo ni ubakaji pamoja na mauaji.

Wapiganaji wa LRA wamejipatia sifa ya kuwatendea unyama wananchi wa kawaida katika maeneo ya kivita kaskazini mwa Uganda. Miongoni mwa unyama huo,ni kuwakata midomo,ndimi na masikio ya wananchi wa kawaida.Pia wanasemekana kuwa wamewachukua mateka vijana maelf kadhaa,huku wakiwageuza vijana wa kike kama wake zao na wakiume aidha kama wapiganaji ama kama watumwa.

Mahakama za kijadi zitatumika

Rais Museveni aliwambia, waliokuwa wamesikilaza, kuwa mpango wa amani na kundi hilo utawasaidia wapiganaji hao kwa kile alichoita kuepuka jela, kwani watahukumiwa na mahakama za kijadi ambazo zinaitwa Mato put.

Rais Museveni ,akiwa jiji London, ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, viongozi kadhaa mkiwemo wale wakijadi, wazee wa hekima,wazee wa mabaraza na pia wahanga wa visa vya wapiaganaji hao kuwa, wapiganaji hao wahukumiwe katika mahakama za kijadi kwa kujibu wa amani.

Rais Museveni amenukuliwa akisema kuwa ikiwa jamii inataka hivyo ni kwanini waipinge.

Chini ya mpango huo wa mahakama za kijadi-Mato Put, kile viongozi wa LRA wanachopashwa kufanya ni kuomba msahama hadharani kutokna na makosa yao na pia kulipa fidia kwa viongozi wa kijadi au wazee.

Lakini hatua hiyo,huenda ikawa kizungumkuti kwa mahakama ya kimataifa ambayo iliundwa mwaka wa 2002 kama mahakama ya kwanza ya kimataifa kushughulikia uhalifu wa kivita.Mahakama hiyo inaweza kulaumiwa kwa kushurutishwa na siasa ikiwa itatupilia mbali kadai hayo ama kukwamisha mazungumzo ya amani ikikataa kufuta kesi hiyo.

Museveni kwa upande mwingine amesema kuwa huenda wahanga fulani wa mateso ya LRA wasifurahishwe na makubaliano ambayo yanawafanya viongozi hao kuwa huru badala ya kwenda jela.

Mawakili wa LRA mapema wiki hii walikutana na maafisa wa mahakama ya kimataifa mjini The Hague wakiomba kesi hiyo kufutwa.

Mpatanishi mmoja katika mazungumzo ya Juba, amesema kuwa kiongozi wa kundi hilo,Joseph Kony, ataondoka msituni mwezi huu kutia saini mkataba wa amani.

Museveni,ambae ni mwenyekiti wa sasa wa jumuia ya madola ya Commonwealth inayojumulisha mataifa 53, amesema anasubiri kuona ikiwa Kony kweli atakubali kuondoka mafichoni.

Wachambuzi wa masuala ya kisasa wanaamini kuwa Kony, ambae amejificha katika mbuga ya wanyama ya Garamba, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,ndie kiungo muhimu kwa amani ya kudumu ya Uganda.

Lakini waasi baado wanashikilia kuwa mkataba wa amani unategemea mahakama ya kimataifa ya The Hague kwanza kuifuta kesi dhidi ya vingozi wao akiwemo Kony mwenyewe na wengine wawili,ikisemekana kuwa wengine wawili waliuliwa.