1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Waasi wa Tigray waanza kuzisalimisha silaha zao nzito

11 Januari 2023

Waasi wa TPLF leo wameanza kuzisalimisha silaha zao nzito, hatua hiyo ikiwa ni moja ya sehemu muhimu ya makubaliano yaliyotiwa saini zaidi ya miezi miwili iliyopita ili kuumaliza mzozo wa kaskazini mwa Ethiopia.

https://p.dw.com/p/4M0QP
Äthiopien | Kämpfer der Tigray People's Liberation Front
Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Msemaji wa chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF Getachew Reda ameandika katika mtandao wake wa Twitter kuwa waasi hao wamezisalimisha silaha zao nzito kama sehemu ya dhamira yao ya kutekeleza makubaliano ya amani yaliyotiwa saini Novemba 2 mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Reda ameandika kwenye Twitter, "Tunatumai kuwa hatua hii itasaidia kuharakisha utekelezaji kamili wa makubaliano." 

Moja kati ya masharti ya makubaliano hayo ya amani ni pamoja na kuwapokonya silaha waasi hao, kurejesha mamlaka ya shirikisho katika jimbo la Tigray na kufungua tena njia za kupeleka misaada na kurejesha mawasiliano katika eneo hilo ambalo limekosa huduma za mtandao na intaneti tangu katikati ya mwaka 2021.

Soma pia: Wanajeshi wa Eritrea wameondoka katika miji mikubwa kaskazini mwa Ethiopia ya Shire na Axum

Hata hivyo, hakukuwepo kauli yoyote kutoka kwa serikali kuu juu ya tamko la TPLF kwamba wameanza kuzisalimisha silaha zao. Msemaji wa serikali hakujibu maombi ya shirika la habari la AFP lililomtaka atoe maoni yake juu ya hatua iliyochukuliwa na waasi wa TPLF.

Mapigano yalizuka mnamo mwezi Novemba mwaka 2020 wakati Waziri Mkuu Abiy Ahmed, alipotuma jeshi huko Tigray ili kuwaangusha viongozi wa Tigray ambao walikuwa wakiipinga serikali yake kwa miezi kadhaa.

Waziri Mkuu huyo pia aliwashutumu viongozi hao wa Tigray kwa kuzishambulia kambi za kijeshi.

Mkataba wa utekelezaji wa amani ulitiwa saini mjini Nairobi

 

Südafrika Pretoria | Friedensgespräche zu Äthiopien, Tigray
Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta akiwasili kwa mazungumzo ya amani kati ya serikali na TPLF mjini Pretoria.Picha: Phill Magakoe/AFP/Getty Images

Mkataba wa utekelezaji wa makubaliano yaliyotiwa saini mjini Nairobi, Kenya mnamo Novemba 12, ulieleza kuwa hatua ya kuzisalimisha silaha za waasi hao utafanyika sambamba na kuondoka kwa vikosi vya kigeni na wapiganaji waliokuwa wakiliunga mkono jeshi la serikali.

Nchi jirani ya Eritrea imekuwa ikiliunga mkono jeshi la Ethiopia katika mzozo huo japo haikushiriki katika mazungumzo ya Pretoria.

Kutokana na njia za kulifikia jimbo la Tigray kufungwa, inaelezwa kuwa ni vigumu kufahamu jinsi hali ilivyo katika eneo hilo la kaskazini mwa Ethiopia. Mfanyakazi wa kutoa misaada anayeishi katika mji wa kimkakati wa Shire ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwa njia ya simu kuwa, amewaona wanajeshi wa Eritrea pamoja na wanajeshi wa Ethiopia katika eneo jirani la Amhara.

Soma pia:UN: Matamshi ya chuki yanachochea vita vya Ethiopia 

Idadi kamili ya vifo vilivyotokana na vita hivyo vilivyodumu kwa miaka miwili, ambavyo kwa kiasi kikubwa viliendelea chini ya vikwazo vikali vya vyombo vya habari, haijulikani japo inaelezwa kuwa vita hivyo viliacha kovu kubwa la mzozo wa kibinadamu.

Vita hivyo vimesababisha zaidi ya watu milioni mbili kukosa makao na kuwaacha maelfu ya wengine wakikaribia kukumbwa na baa la njaa. Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni 13.6 wanategemea misaada ya kibinadamu kaskazini mwa Ethiopia.

Chama cha TPLF chawakabili wanajeshi wa Ethiopia Tigray

Mashirika ya kutetea haki za binadamu likiwemo Amnesty International limeutaja mzozo wa Tigray kuwa "mojawapo ya matukio mabaya zaidi duniani."

Kwa sasa upepo wa matumaini unavuma kwani mapigano hayo yamesimama tangu makubaliano ya amani yaliyopitiwa saini mwezi Novemba, huku waasi wakidai kuwa wamewaondoa karibu asilimia 65 ya wapiganaji wake kutoka uwanja wa mapambano.