1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wauwa wapiganaji 34 wa jihadi Syria

Admin.WagnerD7 Januari 2014

Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria limesema kuwa waasi wa Syria wamewaua wapiganaji 34 wa kigeni walio na mafungano na mtandao wa Al-Qaeda kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1AmVc
Wapiganaji wa jihadi wakifanya gwaride mjini tel Abyad.
Wapiganaji wa jihadi wakifanya gwaride mjini tel Abyad.Picha: Reuters

Taarifa za kuuawa kwa wapiganaji hao wa jihadi zimekuja baada ya vikosi vya jeshi huru ya Syria FSA, kuendesha operesheni dhidi ya makundi yenye msimamo mkali hivi karibuni. Mkuu wa shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London Uingereza Rami Abdul-Rahman, amesema wapiganaji wa jihadi waliuawa katika mji wa Jabal al-Zawya katika siku chache zilizopita.

Mpiganaji wa FSA akijiweka sawa kupambana na wanajihadi.
Mpiganaji wa FSA akijiweka sawa kupambana na wanajihadi.Picha: Reuters

Abdel Rahman alisema wapiganaji waliouawa walichukuliwa mateka baada ya kuanza kwa mapigano kati ya makundi hasimu siku ya Ijumaa. Mapigano hayo ambayo yanayapambanisha makundi ya waasi wasiyo egemea dini na wale wenye msimamo wa wastani dhidi ya wapiganaji wenye mafungano na kundi la Al-Qaeda, yameendelea kaskazini na mashariki mwa Syria, na yamesababisha kuuawa kwa watu kadhaa.

UN haina vyanzo tena vya kuaminika
Wakati waasi wanapigana wenyewe kwa wenyewe ndani ya Syria, msemaji wa ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa Rupert Colville, amesema kushinda kwa ofisi hiyo kutoa takwimu mpya za vifo vinavyotokana na mgogoro huo, kunatokana na kushindwa kwake kufika ndani ya Syria, na kutoweza kuhakiki vyanzo vya taarifa kutoka kwa mashirika mengine.

Colville alisema jumla ya vifo vilivyokadiriwa na Umoja wa Mataifa, ilitolewa kwa kukusanya takwimu sita kutoka mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali katika kanda hiyo. Alisema kadiri siku zilivyokwenda idadi ya mashirika hayo ilipungua hadi kufikia mawili au matatu katika mwaka uliyopita, na hivyo hawakuona kuwa ilikuwa inawezekana kwao kuendelea kutoa takwimu hizo kama kawaida.

Lakini alisema Umoja wa Mataifa haungeweza kuidhinisha takwimu za vyanzio vingine, zikiwemo za shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria, ambalo hunukuliwa na vyombo mbalimbali duniani. Shirika hilo limetoa takwimu zake za hivi karibuni ambazo zinaonyesha kuwa idadi ya waliouawa imefika 130,000.

Mpiganaji wa FSA akiwa kazini.
Mpiganaji wa FSA akiwa kazini.Picha: Reuters

Dola bilioni moja zahitajika kusaidia watoto
Na kwingineko mashirika ya Umoja wa Mataifa na makundi ya misaada yamesema leo kuwa yanahitaji kiasi cha dola bilioni moja kutoka kwa wafadhili ili kuwasaidia watoto wa Syria walioathiriwa na mgogoro huo. Zaidi ya wakimbizi milioni moja wa Syria ni watoto, ambao wengi wao wamepoteza wazazi wao, kujeruhiwa, haki zao kukiukwa, kufanyishwa kazi au kutumikishwa jeshini.

Michango hiyo ya programu iliyopewa jina la kizazi kilichopotea, itatumika kutoa msaada wa kisaikolojia, kuwasomesha watoto walioacha shule, kuwapa mafunzo waalimu na kufadhili miradi mingine.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae, ape,rtre
Mhariri: Mohammed Khelef