1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Uingereza waiweka pabaya Ulaya

Mohammed Khelef
16 Januari 2019

Uamuzi wa bunge la Uingereza kuyakataa makubaliano ya nchi yao kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya umezuwa mtafaruku mkubwa miongoni mwa wanasiasa na wanadiplomasia, huku wengine wakitaka Uingereza iendelee kuwa mwanachama.

https://p.dw.com/p/3BdGI
London Brexit Protest Rettungsring
Picha: Reuters/T. Melville

Mkuu wa timu ya upatanishi wa Umoja wa Ulaya kwenye mazungumzo ya Brexit, Michael Barnier, alikiita kitendo cha bunge la Uingereza kuyakataa kwa kishindo makubaliano yake na Waziri Mkuu Theresa May kuwa ni cha kusikitisha sana licha ya kusema anayaheshimu maamuzi ya wabunge hao

"Daima tumeheshimu na tunaendelea kuheshimu mjadala wa kidemokrasia kwenye bunge la Uingereza na sitaweza kwa sasa kukisia athari za kura hii. Lakini kura ya jana imeonesha kwamba hali ya kisiasa kwa ajili ya kuidhinishwa makubaliano ya Uingereza kujiondoa bado haijawa sawa London", mpatanishi huyo wa Umoja wa Ulaya aliliambia bunge la Ulaya mjini Strasbourg siku ya Jumatano (16 Januari).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas, alisema kwamba hakuna sababu yoyote ya kuchelewesha hatua ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya, hata baada ya makubaliano ya Brexit kukataliwa bungeni. Maas amewaambia waandishi wa habari mjini Frankfurt siku ya Jumatano kwamba baada ya miaka miwili ya kusaka makubaliano ya kujitowa, haoni kuwa kuna chengine kinachoweza kufanyika.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte alionya leo kwamba muda uliobakia ni mdogo sana kwa pande hizo mbili kufikia makubaliano kabla ya tarehe ya mwisho ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya na, kwa hivyo, ameitaka Uingereza kujitafakari tena kwa makini.

"Ni wakati wa Waingereza kuonesha kile wanachokitaka. Muda tulionao ni mdogo sana na unaelekea kwisha," waziri mkuu huyo aliwaambia waandishi wa habari mjini The Hague siku ya Jumatano, akiongeza kwamba bado wanatarajia kufikia makubaliano kabla ya Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi Machi.

Miito ya kura mpya ya maoni

Brexit Theresa May nach Abstimmungsniederlage
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May baada ya kushindwa kwenye kura bungeni.Picha: picture-alliance/empics/PA Wire

Baadhi ya wabunge wa Umoja wa Ulaya waliitolea wito Uingereza kurejesha wazo la kura nyengine ya maoni ili kuwauliza wananchi endapo bado wanataka kuondoka kwenye Umoja huo.

Mkuu wa Umoja wa Ulaya, Donald Tusk, aliashiria kwamba mgawanyiko ndani ya Uingereza hivi sasa huenda ukapelekea kufutwa kwa makubaliano ya nchi hiyo kujiondoa kwenye Umoja huo.

Hata hivyo, Nigel Farage, kiongozi wa zamani wa chama cha UK Independence ambacho kilikuwa kinara wa kampeni ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya mwaka 2016, aliwaambia wabunge wenzake wa Umoja wa Ulaya kwamba kura nyengine yoyote ya maoni itakuja na matokeo mabaya kabisa kwa Ulaya.

"Waingereza watakaomua kujiondoa kwenye Umoja huo watakuwa wengi zaidi, kwa vile walivyochukizwa na misimamo ya Brussels wakati wa majadiliano," alisema Farage.

Tayari, kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour nchini Uingereza, Jeremy Corbyn, ameshatangaza azma yake ya kuwasilisha pendekezo la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Theresa May, mara tu baada ya May kushindwa kwenye kura ya hapo jana.

Wabunge 432 waliyakataa makubaliano yake ya Brexit, kwa 202 walioyaunga mkono, pigo kubwa kabisa kwenye historia ya karibuni ya siasa za Uingereza. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo