1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachezaji nyota watakaokosa dimba la Brazil

9 Juni 2014

Kila mpenzi wa mpira wa kabumbu duniani angependa kuona mchezaji anayemvutia kwa kusakata kandanda duniani akishiriki michuano ya kombe la dunia, lakini kuna wale nyota watakaokosa dimba la Brazil.

https://p.dw.com/p/1CF4H
Zlatan Ibrahimovic
Picha: imago sportfotodienst

Ifuatayo ni orodha ya wachezaji ambao pengine wengi wasingepena kuona wakikosekana katika michuano hiyo ya dunia.

Tukianza na golini tunakutana na Peter Cech mlinda mlango wa Jamhuri ya Czech, Cech ambaye anaichezea klabu ya Chelsea ya Uingereza, anafahamika kwa uwezo wake mkubwa wa kuokoa mashuti makali, kupanga safu yake ya ulinzi lakini pamoja na kuwaongoza wachezaji wenzake kwa ujumla lakini licha ya kuwa na uzoefu mkubwa wa kuichezea timu yake ya taifa ya Czech michezo 107 lakini hakuweza kuivusha katika michuano hiyo ya dunia baada ya kutolewa wakati wa michezo ya kuwania kufuzu.

Katika nafasi ya ulinzi tunakutana na wachezaji nyota kadhaa akiwemo David Alaba wa Austria ambaye ameiwezesha klabu yake ya Bayern Münich kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Ujerumani na kombe la ligi. Umahiri wake uwanjani haukuweza kuifanya timu yake ya Austria imalize katika nafasi ya kwanza katika kundi lake la kuwania kufuzu kucheza kombe la dunia ambalo lilikuwa pamoja na timu ya Ujerumani na Sweden.

David Alaba
David Alaba anasalia kutulizwa na muziki baada ya Austria kushindwa kufuzuPicha: imago sportfotodienst

Lukasz Piszeczek ambaye ni mlinzi wa kulia, uwezo wake uwanjani ulishindwa kuiwezesha Poland kushiriki katika fainali za mwaka huu licha ya kwamba aliisaidia kwa kiasi kikubwa klabu yake ya Borussia Dortmund kutwaa mara mbili kombe la ligi kuu ya Ujerumani.

Mehdi Benatia wa Morocco ni moja kati ya walinzi mahiri kwa sasa wa kati duniani, Benatia ambaye anaichezea klabu ya As Roma itambidi aangalie fainali za dunia za mwaka huu kama shabiki wa kawaida baada ya Simba wa milima ya Atlas yaani Morocco kushindwa kufuzi kwa fainali za dunia za mwaka huu.

Akiwa ameichezea klabu yake ya Borussia Dortmund zaidi ya michezo 150 katika umri wa miaka 25, Neven Subotic ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara mwaka huu, hatoweza kushiriki fainali za dunia baada ya Serbia ambayo ndilo taifa lake kukubali kipigo kutoka kwa Croatia katika mchezo wa mwisho wa mtoano wa kushiriki kombe la dunia.

Gareth Bale
Gareth Bale amekuwa hatari sana msimu uliokamilika, lakini hana fursa ya kucheza katika Kombe la DuniaPicha: imago sportfotodienst

Moja kati ya viungo wanaochipukia kwa kasi kwa sasa ni Thiago Alcantara, umahiri wake uwanjani tokea alipokuwa katika klabu ya Barcelona na sasa Bayern Münich ulimfanya kocha wa mabingwa watetezi wa kombe la dunia Uhispania, Vicente Del Bosque kumjumuisha katika kikosi cha wachezaji 23 kitakachokwenda Brazil katika fainali za dunia lakini kwa bahati mbaya jina la kiungo huyo lilikuja kuondolewa kutokana na kukabiliwa na majeraha hivyo kuzima ndoto yake ya kushiriki fainali za dunia tena katika nchi ambayo wazazi wake wanapotokea.

Baada ya kuchangia kwa kiasi kikubwa klabu yake ya Arsenal kuondokana na ukame wa vikombe kwa kuiwezesha kutwaa kombe la FA, mashabiki wengi wa Arsenal na wengineo wangependa kumuona Ramsey akionesha ufundi wake katika michuano ya kombe la dunia lakini mambo yamekuwa magumu kwake baada ya timu yake ya taifa ya Wales kushindwa kufurukutwa kama kawaida yake inapokuja wakati wa michuano mikubwa ya soka ya ulaya au dunia.

Kama ilivyo kwa Ramsey, Gareth Bale ambaye nae ni raia wa Wales hatokuwemo miongoni mwa nyota watakaokuwa wanatoa jasho uwanjani kutetea nchi zao katika fainali za dunia. Mashabiki wa soka watakosa mengi kutoka kwa Bale ambaye ni mchezaji ghali kuliko wote duniani, kasi yake uwanjani, mashuti yake makali lakini uwezo wake pia mkubwa wa kupiga mipira iliyokufa ndiyo ambayo kwa kiasi kikubwa iliyoiwezesha Real Madrid kutamba katika ligi ya mabingwa wa ulaya.

Ni ngumu kuamini kwa mashabiki wa mabingwa wa dunia wa mwaka 1998 Ufaransa kama watamkosa winga wake mchachari Frank Ribery ambaye ni mchezaji bora watatu duniani baada ya Christiano Ronaldo na Lionel Messi. Jina la Ribery liliondolewa katika orodha ya wachezaji wa Ufaranda wanaoelekea Brazil katika dakika za mwisho baada ya vipimo kuonesha itachukua wiki kadhaa mchezaji huyo kupona majeraha yanayomsumbua hivyo hawezi akashiriki katika michuano ya kombe la dunia mwaka huu. Kila kocha ambaye anaifundisha timu katika fainali za kombe la dunia za mwaka huu angetamani kuwa na mchezaji anayejua fika wapi goli lilipo na ambaye haleti masihara pindi anapokuwa katika nafasi ya kufunga kama Ramadel Falcao wa Colombia ambaye alivunja rekodi iliyowahi kuwekwa na Jürgen Klinsmanns ya kufunga magoli 15 katika mechi 17 za kombe la klabu bingwa ulaya na lile la Europa. Licha ya kukabiliwa na maumivu ya muda mrefu ya goti lakini pia kitendo cha mashabiki mbalimbali wa soka duniani kumuombea apone haraka, Falcao hatoweza kushiriki katika fainali za mwaka huu baada ya kuonekana kuwa hatokuwa katika uwezo wake wakai wa fainali hizo.

Frankreich Nationalmannschaft Franck Ribery
Franck Ribery amesumbuliwa sana na majeraha msimu uliopita wakati akiichezea klabu yake ya Bayern MunichPicha: picture alliance/dpa

Zlatan Ibrahimovic ni mmoja kati ya washambuliaji wachache duniani waliojaaliwa kuwa na uwezo mkubwa wa kufunga magoli, kutengeneza lakini pia kumiliki na kuuchezea mpira jinsi anavyotaka.

Ndoto ya Ibrahimovic ambaye ni raia wa Sweden kushiriki katika fainali za dunia za mwaka huu zilizimwa na nyota mwenzake Christiano Ronaldo wakati Ureno na Sweden zilipocheza katika mechi ya mtoano wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za dunia nchini Brazil.

Nyota wengine ambao watakosa michuano hiyo ya kombe la dunia nchini Brazil ni Theo Walcott wa Uingereza, Riccardo Montolivo wa Italia, Robert Lewandowski wa Poland, Henrikh Mkhitaryan wa Armenia, Christian Eriksen wa Denmark, Marek Hamsik wa Slovakia, Christian Benteke na wengineo.

Mwandishi: Anuary Mkama/AFP/Reuters/DW
Mhariri: Bruce Amani